Viongozi klabu za waandishi wa habari nchini watakiwa kujitathmini

Rais wa klabu za waandishi wa habari Nchini (UTPC),  Deo Nsokolo akizungumza na viongozi wa klabu za waandishi wa habari kutoka mikoa ya Arusha, Manyara, Kilimanjaro na Tanga 

Na Seif Mangwangi, Morogoro

VIONGOZI wa klabu za waandishi wa
habari nchini wametakiwa kufanyia mabadiliko ya Uongozi  klabu zao ili
kuendana na mabadiliko yanayoendelea kufanywa na sekretarieti ya Muunganiko wa
umoja wa klabu hizo nchini (UTPC).


Akizungumza na viongozi wa klabu za
waandishi wa habari kutoka Mikoa ya Kanda ya Kaskazini yenye mikoa ya Arusha,
Manyara, Kilimanjaro na Tanga wanaohudhuria mafunzo ya Uongozi na usimamizi wa
fedha Mkoani hapa, Rais wa Klabu za waandishi wa habari nchini Deo Nsokolo
amesema bila kufanyia mabadiliko ya Uongozi kuna baadhi ya klabu zitanyimwa fedha
za kujiendesha.

Viongozi wa klabu za waandishi wa habari kutoka Mikoa ya kanda ya Kaskazini wakifuatilia mada iliyokuwa ikiwasilishwa na mtoa mada (hayuko pichani)
Mwezeshaji Nice Lema akiwasilisha moja ya mada ya matumizi bora ya fedha katika mafunzo kuhusu utunzaji wa fedha na utawala yanayoendelea Mkoani Morogoro

Amesema moja ya mabadiliko
yanayotakiwa kufanywa na klabu za waandishi wa habari ni pamoja na kuhamasisha
waandishi wengi zaidi wanajiunga uanachama katika klabu zao ili kuboresha umoja
wa waandishi nchini.


“Tunataka mabadiliko makubwa
yafanyike katika siku za usoni, mmeletwa hapa kwa ajili ya kukumbushwa majukumu
yenu katika Uongozi na lengo kuu tunalotaka ni kuboresha waandishi wetu lakini
tutaboresha hali zao wakiwa ndani ya vyama vyetu,”amesema.


Nsokolo amesema moja ya mkakati wa
kuhakikisha idadi ya wanachama inaongezeka ni kuangalia masharti ya kujiunga
ili kuyafanyia marekebisho iwapo yataonekana magumu “uhai wa chama ni wanachama,
inasikitisha kuona klabu ina wanachama ishirini wakati waandishi wa habari waliopo
nje ya klabu ni zaidi ya Hamsini, nashauri nendeni mkaangalie mashrti yenu kama
ni magumu myarekebishe”.


Amesema kwa sasa UTPC imebadili
utaratibu wa utoaji wa fedha kwa klabu kwamba klabu itapewa fedha kulingana na idadi
ya wanachama “Hivi kweli ni sahihi tutoe kiwango cha fedha sawa kwa klabu zote
wakati kuna klabu zina wanachama 20 na nyingine zina wanachama 90?, hii
haliwezekani kabisa, mbadilike ili muende sawa na kasi ya UTPC” alisema Nsokolo

Nsokolo amesema viongozi wanapaswa
kuwa wamoja na wawazi kwa kila taarifa inayohusu klabu ili kuepusha migogoro
isiyokuwa ya lazima ambayo imekuwa ikififisha maendeleo ya klabu nyingi za
waandishi wa habari nchini.


Awali akifungua mafunzo hayo,
Mwenyekiti wa klabu ya waandishi wa habari Arusha ambaye pia ni mjumbe wa bodi
ya wakurugenzi ya UTPC, Claud Gwandu aliwataka viongozi wa klabu kufuatilia
mafunzo hayo kwa makini ili kuivusha UTPC kutoka bora na kuwa bora zaidi.

Mwenyekiti wa klabu ya waandishi wa habari Arusha Claud Gwandu akitoa hotuba ya ufunguzi wa mafunzo ya fedha na utawala kwa viongozi wa klabu za waandishi wa habari katika mikoa ya kanda ya kaskazini