Na Editha Karlo,Kigoma
Wabunge wa mkoa Kigoma wameeleza kuridhishwa na utekelezaji wa miradi mbalimbali inayotekelezwa chini ya mpango wa pamoja Kigoma (KJP) chini ya mashirika 16 ya Umoja wa Mataifa na kwamba miradi hiyo imeleta faida na mabadiliko makubwa kwa jamii.
Mwenyekiti wa wabunge wa mkoa kigoma, Daniel Nsanzugwanko alisema hayo alipokuwa akiongozi timu ya wabunge wa mkoa huo na wajumbe wa kamati ya ushauri ya mkoa Kigoma kutembelea na kukagua miradi inayotekelezwa chini ya mpango wa pamoja Kigoma (KJP) inayotekelezwa na mashirika 16 ya Umoja wa Mataifa.
Nsanzugwanko akizungumza wakati wa ziara ya kutembelea miradi hiyo alisema kuwa ametembea na kuona miradi mikubwa na yenye manufaa makubwa kwa wananchi ikiwamo miradi ya elimu, maji, uwezeshaji , ujenzi wa masoko ya mpakani na uanzishaji wa shughuli za wananchi kiuchum ambayo ina tija baadhi kubwa katika kiinua maisha ya wananchi kiuchumi.
Alisema kuwa pamoja na kazi kubwa iliyofanywa bado miradi mingi haifahamiki kwa viongozi na jamii hivyo kutaka taarifa zake ziwe zinatolewa kwenye vikao mbalimbali vya kiserikali kama ambavyo zinatolewa taarifa za miradi inayotekelezwa kwa fedha za serikali na taarifa hizo zipatikane kwa wakurugenzi ili viongozi mbalimbali wanaotaka taarifa hizo waweze kuzipata kwa urahisi.
Naye Mbunge wa jimbo la Kasulu Vijiji, Augustino Vuma alisema kuwa ipo miradi mikubwa ambayo ina manufaa makubwa kwao lakini baadhi ya miradi hiyo hawakuwa wanaijua kabisa na ziara hiyo imewafungua macho na kuona namna mabilioni ya fedha zinazotumika kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo.
Akizungumza katika ziara hiyo Mratibu wa miradi ya KJP,Evance Siangicha alisema kuwa zaidi ya shilingi Bilioni 100 zinatarajia kutumika kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali chini ya mpango huo na kwamba miradi hiyo imelenga kuleta faida na mabadiliko makubwa kwa jamii ya mkoa Kigoma.
Siangicha alisema kuwa miradi hiyo imeanzishwa ikiwa ni utekelezaji wa mpango wa kuanzisha miradi katika maeneo yaliyoathiriwa na wakimbizi mkoani kigoma kutokana na mkoa huo kuhifadhi idadi kubwa ya wakimbizi wa nchi za maziwa makuu kwa muda mrefu.
Alisema kuwa utekelezaji wa miradi yote imekuwa ikitolewa taarifa kwenye vikao mbalimbali ikiwemo kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa, vikao mbalimbali vya halmashauri na kwa sasa wapo wawakilishi wa Program hiyo katika sekretariet ya mkoa na kwenye halmashauri ambao moja ya kazi zao ni kuwasilisha taarifa za utekelezaji wa miradi hiyo kwenye vikao mbalimbali kwenye maeneo yao.
Mkuu wa wilaya Kasulu, Simon Hanange alisema kuwa ipo miradi mikubwa chini ya KJP ambayo imeanzishwa wilayani humo ikiwemo soko la Mvugwe ambapo litasaidia upatikanaji wa soko la pamoja na kuuzia mazao na kuondoa tatizo la walanguzi kuingia mashambani kwenda kununua mazao hali inayowapunja wakulima.
Mkuu wa wilaya Kibondo Luis Bula alisema kuwa miradi inayotekelezwa chini ya mpango wa pamoja Kigoma (KJP) ni ya manufaa makubwa wilayani humo ikiwemo mradi wa soko la mpakani katika kijiji cha Mkarazi, miradi ya maji katika vijiji vya Kigogo na Nyange wilayani Kibondo miradi ya kilimo cha kisasa na miradi ya ujasiliamali kwa vikundi vya wanawake na vijana