Wafanyabishara arusha watakiwa kutumia kituo jumuishi kurasimisha biashara zao

Kaimu mkurugenzi wa jiji la Arusha akieleza jambo kuhusiana na Kituo jumuishi Cha urasimishaji na uendelezaji wa biashara mbele ya waziri Jenista mhagama

 Na Queen Lema Arusha

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Jenista Mhagama amewashauri na kuwataka wafanyabiashara wadogowadogo mkoani Arusha kutumia kituo jumuishi Cha urasimishaji na uendelezaji wa biashara ambacho kimeanzishwa na mpango wa kurasimisha rasilimali na biashara kwa kushirikiana na jiji la Arusha.

Aidha lengo halisi ni kuhakikisha kuwa biashara za wafanyabiashara hao pamoja na pato la taifa linakuwa kwa kiwango kikubwa sana.

Mhagama aliyasema jijini Arusha wakati akizindua kituo Cha urasimishaji  kilichopo katika Kata ya Kati, Mtaa wa Pangani,

Alisema kuwa lengo halisi la Serikali ni kuhakikisha kuwa kila mara Kuna kuwa na mikakati ya kuweza kuwasaidia wafanyabiashara ambapo sasa kupitia kituo hicho wataweza kupata msaada na ufafanuzi juu ya masuala mbalimbali

 ” kituo hiki kimeanzishwa mahususi kwa ajili ya kuwasaidia wajasiriamali kujifunza mambo mbalimbali pamoja na kupatiwa mbinu tofauti za kibiashara hivyo ni fursa kwao kukitembelea ili kupata huduma hiyo.

“lakini pia kituo kitasaidia kurasimisha biashara zenu na kuweza kutambulika na taasisi za kifedha ili muweze kupata mikopo katika taasisi hizo kwa lengo la kuinua biashara zenu kwa maendeleo yenu binafsi na taifa kwa ujumla,” Mhe. Jenista amesisitiza

Katika  hatua nyingine  waziri huyo aliwataka wajasiriamali Arusha kuhakikisha kuwa wanapata  huduma bora katika kituo hicho, sanjari na taasisi zote zinazotoa huduma jumuishi kushiriki kikamilifu kutoa huduma ili wafanyabiashara hao wasipate au kukutana na changamoto mbalimbali pindi  wanapoenda kupata huduma katika kituo hicho.

Nasisitiza kwa mara nyingine kuwa kupitia mpango wa  MKURABITA  sisi kama Serikali tumeweza fedha nyingi kuanzisha kituo hichi ambacho ni kikubwa chenye ubora, hivyo taasisi zote jumuishi zinatakiwa zitoe huduma na kuondoa kadhia kwa wafanyabiashara hao kwa kuwapatia huduma inayostahili kama ilivyokusudiwa,” Mhe. Jenista amesisitiza.

Awali , Mratibu wa MKURABITA, Dkt. Seraphia Mgembe alisema kuwa bado wana mikakati mbalimbali ambayo wataweza  kushirikiana na Halmashauri ya Jiji la Arusha katika mambo mbalimbali ya kuwawezesha wafanyabiashara hao  waweze kujikwamua kiuchumi 

Alitaja mkakati huo kuwa ni pamoja na kuratibu mafunzo ambayo yataweza kuwapa uelewa juu ya biashara zao.

Kituo Jumuishi cha Urasimishaji na Uendelezaji wa Biashara kimeanzishwa ili kuwasaidia na kuwarahisishia wafanyabiashara wa Jiji la Arusha kupata huduma zote za ushauri wa biashara pamoja na kupata mahitaji yote ya kibiashara katika sehemu moja.