Wajasiriamali washauriwa kuzalisha bidhaa bora

 Na Magesa  Magesa,Arusha


WAJASIRIAMALI hapa nchini wameshauriwa kuhakikisha kuwa wanazalisha
bidhaa bora zenye tija na viwango hali ambayo itawasaidia kupata
masoko ya uhakika ya bidhaa zao ndani na nje ya nchi.

Meneja wa Shirika la kuhudumia Viwanda Vidogo(SIDO) Mkoa wa
Arusha,Jalphary Dongealiyasema hayo juzi  alipokuwa
akifunga mafunzo ya usindikaji wa bidhaa za chakula yaliyofanyika
katika ofisi za Shirika hilo Mkoani hapa

“Endapo mtazalisha bidhaa bora,zenye viwango na kuziweka katika
vifungashio bora na kuziuza kwa  gharama nafuu, itawasaidia kupata
soko kubwa na la uhakika la bidhaa zenu ndani na nje ya nchi,nahitaji
kuona wajasiriamali wadogo wanafanikiwa”alisema Donge

Meneja huyo aliwataka wajasiriamali wawe  wabunifu, na
kwamba SIDO
licha ya kuwapatia mafunzo ya ujasiriamali imekuwa ikiwaunganisha na
taasisi mbalimbali zikiwemo za kifedha na kuwataka wachangamkie fursa
hiyo na kuacha kufanya biashara kwa mazoea kwani sokoni kuna ushindani
mkubwa.

“Pangilia vitu vyako vizuri  kwani maisha yako yako mikononi mwako
nataka kuona wale wote wanaopita kuapa mafunzo hapa SIDO wanafanikiwa
hivyo ni nyie kuhakikisha kuwa mnakuwa wabunifiu na kuongeza bidii
katika shughuli zenu ili muweze kufanikisha malengo yenu”alisisitiza
Meneja huyo wa SIDO Mkoani hapa.

Kwa upande wake Afisa uendelezaji wa biashara wa  SIDO Mkoani hapa,

Bahati Mkopi aliwataka wajasiriamali hao kuhakikisha kuwa
wanazingatia mafunzo hayo na kwenda kuyafanyia kazi kwa vitendo ikiwa
ni pamoja na kuwa mabalozi wazuri kwa wajasiriamalia wengine.

Aliongeza kuwa kwa sasa vijana wengi wamekuwa wakikaaa vijiweni na
kulalamika kuhusu ukosefu wa ajira na kuwataka waamke na waache
kulalamika kwa kuchangamkia fursa zilizopo ili kujikwamua kiuchumi kwa
kufika katika ofisi za SIDO ili waweze kupata mafunzo ya ujasiriamali.

Mkopi alisema kuwa mafunzo hayo ni ya wiki moja ambapo
yamewashirikisha wajasiriamali 29 kutoka mikoa ya Arusha,Kilimanjaro
na Mwanza na kwamba walifundishwa usindikaji wa bidhaa za chakula
ikiwa ni pamoja na uongezaji wa thamani wa mazao ya kilimo na mifugo.

Kwa upande wao baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo Rodney Benson na
Rose Werema waliishukuru SIDO kwa kuwapatia mafunzo hayo kwani baada
ya mafunzo hayo wanatarajia kuanzisha viwanda vidogo vitakavyowasaidia
kujikwamua kiuchumi na kujiongezea vipato.

Kwa upande mwingine walieleza changamoto kubwa wanayokutana nayo
katika uanzishwaji wa viwanda vivyo  kukosekana kwa mikopo na pale
inapopatikana imekuwa ikitolewa kwa riba kubwa na kuliomba Shirika
hilo la kuhudumia viwanda vidogo kuwasaidia kupata mikopo  yenye riba
nafuu.