Na Mapuli Misalaba, Shinyanga
Wakazi wa Manispaa ya Shinyanga wameiomba serikali kuendelea kutoa elimu sahihi kwa jamii kuhusu uchukuaji wa tahadhari za kujikinga na virus vya Uviko 19 ili kukabiliana na tishio la mlipuko wa wimbi la nne la ugonjwa huo unaoendelea kuleta athari katika mataifa mengine ulimwenguni.
Wamesema kuwa serikali iendelee kuweka msukumo na usimamizi ili kuhakikisha uchukuaji wa tahadhari unazingatiwa na wananchi wote hasa katika maeneo yenye mkusanyiko.
Wameahidi kuendelea kuiunga mkono serikali inayotaka kuwaepusha wananchi wake dhidi ya janga la Uviko 19 linalosababishwa na Virus vya Corona.
Akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa Barabara ya Morocco –Mwenge jijini Dar es salaam jana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan alitumia nafasi hiyo kuwakumbusha watanzania kuendelea kuchukua tahadhari za kujikinga na tishio la mlipuko wa wimbi la nne la maambukizi ya virus vya Uviko 19.
“Duniani huko kumeanza wimbi la nne la ugonjwa huo wa Uviko 19 au Covid 19 hatuna budu kuchukua kila tahadhari lakini pia serikali imeleta chanjo kwa wale ambao bado hawajachanja nendeni mkachanje kwa sababu kwa wenzetu limeanza na kwa sababu wanadamu tunasafiri tunakwenda basi hatuwezi kuwa na uhakika lini jambo hili litafika kwetu”