Wakuu wa mikoa kusimamia usajili wa wakulima utoaji mbolea ya ruzuku

Na Fred Kibano, Dodoma

Serikali imewaagiza Wakuu wa Mikoa kote nchini kusimamia kwa ukamilifu zoezi la kuwasajili wakulima kwa ajili ya zoezi la Mfumo wa utoaji wa mbolea ya ruzuku kwa msimu wa mwaka huu

Hayo yamesemwa na Mhe. Innocent Bashungwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI wakati akitoa salamu kwenye kikao maalum kati ya Ofisi ya Rais TAMISEMI na Wizara ya Kilimo kilichowahusisha Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa katika ukumbi wa St. Gaspar Jijini Dodoma hivi leo

“lipo suala la wakulima waheshimiwa Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa, ili tuweze kupeleka huduma kwa mkulima, kuna suala la kusajili wakulima wetu, Wizara ya Kilimo inatutegemea sisi ili kuhakikisha suala la kuwasajili wakulima linafanikiwa kwa kiasi kikubwa”

Bashungwa amesema pia lengo la kikao hicho ni sehemu ya kujipanga katika kuhakikisha utekelezaji wa dira na maelekezo ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha yanatokea mapinduzi chanya kwa wakulima kote nchini.

Akitoa hotuba katika kikao hicho, Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe amesema wizara yake inazingatia teuzi za Bodi za Kilimo kuwa na Mkuu wa mkoa kama mjumbe kwani wao pamoja na Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala wa Mikoa ndio kama mikono ya wizara ya kilimo na lazima wahusishwe kwenye masuala yote ya kilimo kwenye maeneo yao.

Aidha, Bashe amesema katika mwaka wa fedha 2022/2023 Wizara ya Kilimo itaajiri Wahandisi wa umwagiliaji ambao watapelekwa katika kila halmashauri zoezi ambalo litakwenda sambamba na kuwapatia magari kwa ajili ya ufuatiliaji wa kazi zao

Katika hatua nyingine Waziri Bashe amesema Wizara yake inatarajia kujenga maghala 62 mapya kwa ajili ya kuhidhia mazao ambapo mkoa wa Ruvuma utakuwa na maghala 31sawa na asilimia 80 ya maghala yote.  

Akiongea kwa niaba ya Wakuu wa Mikoa Mwenyekiti wa Wakuu wa Mikoa ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. John Mongela amesema kuwa suala la wakulima ni sehemu ya jukumu lao na hivyo watalitekeleza kama ilivyoagizwa.

Kikao kazi hicho cha siku moja kilikuwa na lengo la kuwakutanisha Viongozi hao na wizara mbili ili kuona namna ya kumsaidia mkulima nchini na kukuza ustawi wa uchumi wa mazao kwa ujumla.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *