Wamiliki wa magari watakiwa kupeleka magari yao polisi kwaajili ya ukaguzi

 Na Mapuli Misalaba, Shinyanga

Mkuu wa usalama Barabarani wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga Mrakibu wa Polisi Malege Emanuel Kilakala amewakumbusha wamiliki na madereva wa vyombo vya moto kuzingatia kanuni na taratibu zilizopo kwa mujibu wa sheria,ikiwemo kukaguliwa vyombo vyao.

Amesema ni wajibu kwa wamiliki wa vyombo vya moto kupeleka magari yao kukaguliwa na  kuhakikiwa iwapo yamekidhi matakwa ya kisheria juu ya  usalama barabarani ambapo pia madereva  wamekumbushwa kutii sheria bila shuruti hasa kwa kuzingatia  alama mbalimbali ikiwemo vivuko.

“Wamiliki wahakikishe wanapeleka vyombo vyao vya moto kukaguliwa badaye tutapita kuja kukagua lakini madereva turudi katika kuheshimu watumiaji wengine wa barabara tuheshimu alama, michoro, vivuko vya watembea kwa miguu tusianze kuonyesha sasa ule udereva wa kushindana kingine madereva watii sheria bila shuruti”amesema Kilakala

Kilakala ametoa kauli hiyo leo ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya wiki ya nenda kwa usalama Barabarani ambapo amesema Jeshi hilo limeendelea kuelimisha jamii hasa wamiliki,madereva pamoja na watumiaji wa barabara kuhusu sheria,kanuni na taratibu za usalama barabarani kwa kuwa  ndiyo lenye dhamana hiyo hapa nchini.

Kwa upande wao watumiaji wa vyombo vya moto wakiwemo madereva wa magari na pikipiki wameahidi kuongeza umakini na uzingatiaji wa sheria za usalama barabarani ili kudhibiti ajali zinazoweza kuzuilika

Maadhimisho ya wiki ya nenda kwa usalama Barabarani kitaifa Mwaka huu yatafanyika Mkoani Arusha kuanzia Novemba 11,na kilele chake kitakuwa Novemba 20,ambapo kauli mbiu yake inasema “Jali Maisha yako na Watu wengine Barabarani”