Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tawi la Mkombozi, Kata Pangani, Kibaha Mjini mkoani Pwani wamekiomba chama hicho Taifa kuingilia kati uuzwaji ardhi ya chama hicho katika tawi la Mkombozi ili irudishwe mikononi mwa chama.
“Hili eneo ni mali ya CCM, palikuwa na ofisi ya udongo ya CCM, ghafla tunaona pameuzwa, sisi kama wanachama hatujawahi kushirikishwa wala kuulizwa. Tunachofahamu mali za chama zina utaratibu wake, ni lazima upewe kibali na Bodi ya Wadhamini, hili halikufanyika. Tunaomba sana CCM Taifa watusaidie ili ardhi yetu iweze kurudi,” alisema mwanachama mmoja wa CCM.
Wana CCM wanasema kurudishwa kwa ardhi hiyo kutanufaisha sio tu CCM Tawi la Mkombozi kwa kuanzisha miradi mbalimbali, bali kutasaidia kuendeleza chama kwa ujumla, kwani kama ni miradi itaanzishwa au vitega uchumi vitakuwepo, vitakuwa ni mali ya CCM kama chama, sio mali ya tawi.
Baadhi ya wana CCM wameandika barua ofisi ya wilaya Kibaha Mjini wakiomba ardhi yao kurudishwa, wakidai wenye ardhi ni wana CCM chini ya Bodi ya Wadhamini CCM Taifa ambao katika kuuza ardhi hakuna barua waliyotoa kuridhia kuuzwa eneo hilo.
Inadaiwa kuwa hata wakati fulani CCM Taifa ilifanya uhakiki kujua maeneo yake, lakini eneo la ardhi hii lilifichwa, hawakuonyeshwa.
Katibu wa CCM tawi la Mkombozi, Julieth Faustine (pichani juu) anakiri kupokea taarifa ya eneo hilo kuuzwa na kusema anaamini viongozi wa juu wa chama watalishughulikia suala hilo na kulimaliza katika hali ambayo chama kitapata haki yake.
“Liliuzwa kabla sijaingia madarakani. Kama wanavyosema wanachama ni eneo ambalo wanachama wanajua ni mali ya CCM yetu, kwa miaka mingi palikuwa na ofisi ya CCM iliyokuwa imejengwa kwa udongo hapa. Baadae umiliki wa eneo hili inadaiwa uliondolewa mikononi mwa tawi na kuwa mikononi mwa CCM Kata Pangani, huko ndiko walikouza,” anasema Julieth na kuwaomba wanachama wa CCM Tawi la Mkombozi wawe na utulivu.
Kwa mujibu wa kanuni za mali za chama, chochote ambacho ni mali ya CCM hakiwezi kuuzwa pasipo kibali cha maandishi kutoka BODI YA WADHAMINI, na yeyote ambaye anauza pasipo ridhaa ya bodi hiyo ni batili na muuzaji anapaswa kumrudishia fedha zake aliyeuziwa.