Wanafunzi kuanza kutumika kuhamasisha utalii wa ndani

pichani Wanafunzi wanaoishi katika mazingira magumu wakiwa wanatembeleahifadhi ya jamii ya Burunge kujionea vivutio vya utalii ziara ambayo iliandaliwa na taasisi ya chemchem.

pichani Wanafunzi wanaoishi katika mazingira magumu wakiwa wanatembeleahifadhi ya jamii ya Burunge kujionea vivutio vya utalii ziara ambayo iliandaliwa na taasisi ya chemchem. 

Mwandishi wetu.Babati

Wanafunzi wa shule za msingi, sekondari na vyuo mkoa wa Manyara, wanatarajiwa kuanza kutumika kama mabalozi wa kuhamasisha Utalii wa ndani na kupiga pita ujangili baada ya kupatiwa elimu ya Utalii.

Akizungumza na kundi la wanafunzi wa kituo cha kulea  watoto wanaoishi katika mazingira magumu cha Mdori wilayani Babati, Mwongoza watalii wa Taasisi ya chem chem ambayo imewekeza shughuli za Utalii,katika eneo la hifadhi ya wanyamapori ya Burunge,  Salum Mpampa alisema wameamua kuanza kuhamasisha wanafunzi kupenda utalii na uhifadhi ili waje kuwa mabalozi katika sekta hiyo.

“kundi hili la wanafunzi kutoka kituo cha  TGCWC ni mfululizo ya makundi ya wanafunzi ambao tumeanza kuwaleta kutembea hifadhi hii ili kujionea faida za utalii lakini pia kutambua rasilimali ambayo mungu amelijalia taifa hili kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo”alisema

Alisema wanafunzi hao, wanapata fursa kuona wanyama mbali mbali, kupata elimu ya uhifadhi katika kitalu cha EBN lakini pia wanapata fursa ya kuuliza maswali kuhusiana na masuala ya uhifadhi.

Mpampa alisema katika hifadhi hiyo, Chemchem wamekuwa wakifanya utalii wa picha lakini pia wanahuduma za kambi za watalii na hoteli ya kitalii.

Mlezi wa kituo hicho, Sipora Paulo alisema wamejifunza mambo mengi katika hifadhi hiyo, ambayo ipo kati kati mwa hifadhi ya Tarangire na Manyara.

“tumeona wanyama wengi sana, tumejifunza maisha yao lakini tumeona faida ya uwekezaji wa taasisi ya chemchem katika hifadhi hii”alisema.

Hivi karibuni, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constatine Kanyasu alitembelea hifadhi hiyo na kuwashauri wawekezaji na uongozi wa hifadhi ya jamii ya Burunge, kuanza mikakati ya kuhamasisha utalii wa ndani ili kuwavutia watu wengi kutembelea vivutio vya Utalii katika eneo hilo.