*waratibu klabu za waandishi wa habari wanolewa kuhusu haki za binaadam *watakiwa kuibua vitendo vya kikatili wanavyofanyiwa waandishi

Na Seif Mangwangi, Dodoma

WARATIBU wa klabu za waandishi wa habari nchini, wametakiwa
kuongeza jitihada za kufuatilia matukio ya ukiukwaji wa haki za binaadam dhidi
ya waandishi wa habari na kuripoti kwaajili ya kuchukuliwa hatua.

Akifungua mafunzo ya siku tatu kwa waratibu hao jana Jijini
Dodoma, Afisa Programu kutoka klabu za waandishi wa habari nchini UTPC, Victor
Maleko amesema waandishi wa habari wamekuwa wakikabiliwa na ukiukwaji wa haki
za binaadam na kukwamisha utendaji wao wa kazi wa kila siku.

Amesema UTPC kwa ushirikiano na shirika la IMS Denmark wameingia
mkataba wa kusimamia ukiukwaji wa uhuru wa habari (madhila),  ambayo ni moja ya haki za msingi za kidunia
na  waratibu kwa kuwa ni kiungo kikubwa
wanatakiwa kuongeza juhudi za kuripoti matukio hayo ili kuyakomesha.

Maleko amesema ili kufanikisha zoezi hilo UTPC imekuwa ikitoa
mafunzo na midahalo mbalimbali ya ulinzi na usalama kwa mwandishi wa habari
ikiwemo waratibu kujengewa uwezo wa kufwatilia madhila dhidi ya waandishi wa
habari nchini.

“Leo mko hapa kwaajili ya kujengewa uwezo wa namna bora kufuatilia
ukiukwaji wa haki za kupata taarifa na uhuru wa habari ikiwemo madhila dhidi ya
waandishi wa habari, tunaamini baada ya mafunzo haya mtarudi kazini mkiwa mko
vizuri kuripoti matukio ya ukiukwaji wa haki za binaadam kwa waandishi wa
habari,”amesema.

Akiwasilisha mada kuhusu uhuru wa kujieleza na akitumia
uzoefu wake kitaifa, Wakili John Sendodo amesema ili kuweza kutambua haki za
msingi za binaadam ni vyema kujua haki za kimataifa na namna nchi zingine
zimekuwa zikitekeleza haki hizo.

Pia amesema kumekuwepo na mikataba ya kimataifa kuhusu haki
za binaadam ambayo Tanzania ni miongoni mwa mwanachama wake hivyo ni vyema
waratibu wakaelewa na kujua mipaka yao wakati wa kuripoti matukio hayo.

Kwa upande wake mwakilishi kutoka shirika la IMS Zimbabwe, Rashweat
Mukundu ametoa uzoefu wake kuhusu madhila yanayotokea Zimbabwe na kuwataka
waratibu hao kuwa makini wakati wa kuchambua madhila hayo kwa kuwa wanaoyafanya
na wao hutumia akili nyingi sana.

“Nchini Zimbabwe waandishi wa habari wanafanyiwa sana madhila
lakini kama hauko makini unaweza usibaini ukweli wa tukio lililotokea, hivyo
mbinu mbalimbali zinahitajika ili kuweza kubaini,”amesema.

Pia amewataka waratibu kuripoti haraka matukio ya madhili
pindi yanapotokea ili kurahisisha upatikanaji wa mwandishi aliyetendewa tukio
husika lakini pia kufanya uchambuzi wa kina na kubaini ukweli ili kuepuka
mgogoro usiokuwa wa lazima na mamlaka za kiserikali.