Wataalam wa tiba waanza kusaka dawa ya corona

Wataalam tiba asili wakiwa wameshikilia dawa wakijiandaa kuiwasilisha kwa mwakilishi wa mkuu wa mkoa

Na Mustafa Leu, Arusha 

WATAALAM wa tiba asili nchini, wamejitosa kusaka tiba na dawa ya kukinga na kutibu virusi vya ugonjwa wa mlipuko wa Covid-19 ambao umeikumba dunia tangia mwanzo mwa mwaka huu 2020  ugonjwa ambao hajapatikana  tiba wala chanjo.

Wataalam hao kutoka mikoa mbalimbali kwa nyakati tofauti na mazingira tofauti kila mmoja kwenye eneo lake analoishi  ameingia msituni kusaka dawa ya kutibu ugonjwa huo, wa Covid -19 au Corona.

Wataalam hao kupitia Chama chao cha tiba asili Chawatiata( T ) kutoka mikoa mbalimbali nchini hivi karibuni wamekutana jijini Arusha ambapo waliweka kambi ya wiki moja kwa ajili ya kuwasilisha dawa zao hizo wanazoziamini kwa mkemia mkuu wa serikali .

Wametia kambi kwenye ofisi ya Chama cha Mapinduzi,CCM,kata ya Daraja mbili  ambapo wamewasilisha dawa zao hizo kupitia ofisi ya mkuu wa mkoa wa Arusha..

Mkurugenzi mkuu wa Chama hicho,Cha Chawatiata (T) Daud Nyaki,anasema dawa hizo wamezipeleka kwa mkemia mkuu wa serikali ili kujiridhisha na kuona kiwango cha ubora wake na uwezo wa kutibu kwa sababu ni mkusanyiko na mchanganyiko wa miti mbalimbali .

Anasema wataalamu hao wamekubaliana kupitia Chama chao kwamba kila mtaalam wa tiba asili awasilishe dawa zake kabla ya kuzitumia ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza.

3Kila mmoja aliichuma majani,kuchimba mizizi na kuchuna au kubandua magome  ya miti na kisha kutoka na mzigo wa kutosha kwa ajili ya kutolea matibabu kwa wagonjwa wa Covid-19.

Amesema mlipuko wa magonjwa kama hayo umekuwepo ulimwenguni ila kwa nyakati tofauti hutokea na wataalam wa tiba asili wamekuwa wakitumika kutafuta tiba  na wamekuwa wakifanikiwa.

Anasema hatua ya kuzipeleka kwa mkemia mkuu ni pamoja na kuingezea thamani na ubora na hivyo kuondoa dawa ambazo ni sumu au zinaweza kuleta athari kwa afya ya mtumiaji.

Anasema wataalam hao baada ya kuchuna au kubandua magome ya miti ,kuchimba mizizi huwa wanaikausha na kisha kuichanganya na kusaga unga ambao ndio wameupeleka kwa mkemia mkuu.

Anasema huo ni mwendelezo wa matumizi ya tiba asili ya kujifukiza na kupiga nyungudhidi ya ugonjwa wa Covid -19 ambao maelfu ya watu hasa wazee wamepoteza maisha.

Hapa  nchini kwetu ugonjwa huo ulilipuka mwezi Marchi baada ya mtanzania mmoja (Isabela Mwampamba, ) aliyeambukizwa virusi vya Corona alipokuwa akitokea nchini Ubeligiji.

Alipofika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro, Mwampamba,alipanda taxi kutoka uwanjani hapo hadi hoteli ya Pepe iliyopo eneo la Uzunguni jijini Arusha, na kisha alipelekwa hospital ya Mount Meru kwa matibabu ambako kulikuwa kuna eneo lililotengwa rasmi kwa ajili ya walioambukizwa Covid.

Maambukizi ya ugonjwa huo yaliendelea kusambaa na kuenea kwenye baadhi ya mikoa kutokana na mwingiliano wa wageni wengi kuingia nchini wakitokea kwenye nchi zenye maambukizi .

Ugonjwa huo wa Covid umeathiri uchumi wa nchi na  uchumi wa mtu mmoja mmoja . Katika kipindi cha  karibuni ugonjwa huo ambao maambukizi yake yalikuwa yameanza kupungua,umeibuka tena  ulimwenguni.

Nchi ambazo zimeathiriwa sana na maambukizi ya ugonjwa huo ni pamoja na Marekani, Italia, Ubeligiji, Ufaransa,Hispania , India,China, Ujerumani ,Uingereza ,ambapo maelfu ya watu wengi wenye umri mkubwa wamepoteza maisha.

Hivi karibuni Ulimwengu umeshuhudia waziri mkuu wa Uingereza Borris Johnson, akiugua ugonjwa huo,pia rais  wa Marekani, anaemaliza muda wake Donard Trump  nae akipata maambukizi ya ugonjwa huo wa Corona.

Kutokana na kuzuka upya kwa ugonjwa huo  ni jukumu la kila mmoja wetu kuishi kwa kuchukua tahadhari  kwa kuzingatia kanuni na ushauri wa wataalam wa afya.

Huku msisitizo ukiwa ni kuishi wa kuepuka misongamano isiyokuwa ya lazima, kunawa mikono kila wakati mara baada ya kugusa kitu au kushikana mikono  na mwenye kupiga chafya au kukohoa lazima akinge na mikono yake ili kuzuia maambukizi kwa mwingine.