Watakiwa kutoa maoni badala ya kulalamika

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko

 Na Mapuli Misalaba, Shinyanga

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Bi. Jasinta Mboneko amewataka wadau wa maji kujenga utamaduni wa kutoa maoni na ushauri kwa Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Shinyanga SHUWASA ili kuboresha huduma zake,badala ya kulalamika.

Mboneko ametoa wito huo leo wakati akifungua warsha ya wadau wa maji walioketi  kupitia rasimu ya Mkataba wa huduma kwa wateja ambayo imefanyika katika ukumbi wa ofisi ya mkuu wa mkoa wa Shinyanga.

Mboneko amesema kuwa dhana ya kuwa na mkataba wa huduma kwa wateja inatokana na ukweli kwamba utoaji wa huduma ya maji safi kwa wananchi una changamoto nyingi na kwamba zinahitaji juhudi za pamoja katika kuzitafutia ufumbuzi.

“Lazima sisi tuwe mstari wa mbele kuishauri mamlaka ifanye vizuri kulikoni kutoa lawama desturi yetu sisi watanzania ni kulaumu tu lakini hatuko tayari kutoa ushauri nafikiri sasa tubadilike tuwe ni wakutoa ushauri kuliko kulaumu niwaombe sana washiriki  tuwe  wajumbe wazuri wakuendelea kuelimisha jamii, kutoa taarifa, kutoa maoniu ili mamlaka ifanye vizuri zaidi”

Aidha Mboneko ameiomba SHUWASA kuongeza kasi ya usambazaji wa huduma hiyo kwenye maeneo anbayo bado hayajafikiwa na huduma hiyo.

Kwa upande wao wadau walioshiriki katika warsha hiyo wameitaka SHUWASA kuboresha utoaji wa huduma zake ikiwemo miundombinu ya maji.

Wametaja changamoto mbalimbali zinazohitaji kutafutiwa ufumbuzi ikiwemo uboreshaji wa miundombinu ya maji,  kupeleka huduma bora ya maji kwenye maeneo yenye uhitaji,lakini pia kutoa elimu sahihi kwa jamii kuhusu wajibu na haki za wateja.