Watendaji halmashauri watakiwa kuhakikisha waliochaguliwa kidato cha kwanza wanaanza masomo

 Na Mapuli Misalaba, Shinyanga

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Sophia Mjema amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri zote Mkoani hapa,maafisa Elimu na watendaji wa Serikali kuhakikisha wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza kwa Mwaka wa Masomo 2022 wanaripoti na kuanza masomo.

Ametoa agizo hilo leo kwenye kikao cha kamati ya ushauri ya Mkoa kilichofanyika  kwenye ukumbi wa mikutano wa jengo la ofisi ya Mkuu wa Mkoa,ambapo pamoja na mambo mengine amesisitiza wanafunzi wote waliochaguliwa kwa Mwaka wa Masomo kuripoti shuleni mara moja.

Mheshimiwa Mjema amesema mpaka ifikapo Machi Mosi,Mwaka huu awe amepokea taarifa ya utekelezaji wa agizo hilo.

“Tushirikiane ipasavyo kwenye suala hili na nitapenda  kupata taarifa ya utekelezaji wa agizo hili kabla tarehe moja mwezi wa tatu Mwaka huu 2022”.

Amesema jumla ya Wanafunzi 29,757 kati yao Wasichana ni 15,827 na Wavulana ni 13,930 wamechaguliwa  kujiunga na kidato cha kwanza kwa Mwaka wa Masomo 2022 katika shule mbalimbali za Sekondari Mkoani Shinyanga.

Aidha katika kikao hicho Mjema  amewasisitiza maafisa  kilimo wa mkoa wa Shinyanga kuendelea kutoa elimu kwa wakulima ili kulima kilimo kwa kufuata kanuni za kilimo pamoja na utumiaji bora wa mbolea ili kuleta matokeo chanya katika sekta ya kilimo.

Wakati huo huo mkuu wa mko wa Shinyanga Mjema amesisitiza  suala la upandaji miti kwa kila Kaya katika ngazi ya wilaya, kata na vijiji ambapo amesema itasaidia kuendelea kuleta mvua lakini pia kupunguza ukame katika mkoa wa Shinyanga. 

Kikao cha kamati ya Ushauri RCC kilichoketi leo ni kikao cha kwanza kwa Mwaka huu 2022 , na kwamba  ni chombo cha kisheria  kinachotoa ushauri wa utekelezaji wa shughuli za serikali za Mkoa.