Watu wasiojulikana wachoma moto ofisi ya mtendaji wa kata ya soweto katika manispaa ya moshi.

Watu wasiojulikana wamechoma moto ofisi ya Serikali ya mtendaji wa kata ya Soweto katika Manispaa ya Moshi.

Taarifa
kutoka eneo la tukio zinaeleza kuwa watu hao walichoma ofisi hiyo kwa
kutumia mafuta ya petroli na kusababisha baadhi ya nyaraka na samani za
ofisi kuungua.


Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Dk. Anna Mghwira, alithibitisha jana
kupokea taarifa za uhalifu huo, muda mfupi baada ya kuzuru eneo la
Wailes, lilipo jengo hilo.

Katika taarifa yake, Mghwira ameagiza kufanyika uchunguzi wa kina ili
kubaini wahusika wa tukio hilo, huku akisema ni mapema mno kulihusisha
na masuala ya siasa.

Watu hao wanadaiwa kuichoma moto ofisi hiyo, Novemba 9, mwaka huu, kati ya majira ya saa 1:30 na saa 2:30 usiku.

“Ni kweli mimi na kamati yangu ya ulinzi na usalama mkoa, nilipokea
taarifa hizo jana usiku kwamba kuna watu wasiojulikana wamechoma Ofisi
ya Mtendaji wa Kata ya Soweto iliyoko eneo la Wailes, Manispaa ya Moshi
na kuunguza nyaraka za serikali.

“Nimesha vielekeza vyombo vya ulinzi na usalama kuanza uchunguzi mara
moja ili kubaini kiini cha uhalifu huo. Mpaka sasa kuna watu kadhaa
wameshakamatwa na wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa ajili ya
mahojiano.”

Kwa mujibu wa Dk. Mghwira, tukio la kuteketezwa kwa ofisi hiyo
liligunduliwa na mtu mmoja aishie jirani na ofisi hiyo, ambaye anadai
kusikia harufu ya petroli na ya vitu vinavyochomwa moto.

“Jirani huyo alihisi kuna taka zinachomwa ndipo akaamua kuchungulia
kupitia dirishani na kuona ofisi ya mtendaji ikiwa imeshika moto, hapo
hapo, ndipo alipotoka nje na kupiga kelele, kitendo ambacho
kilisababisha wananchi wenzake kutoka nje na kuuzima moto huo na kisha
kufanikiwa kupunguza athari zilizoanza kujitokeza,” alisema Mkuu huyo wa
Mkoa.

Pia Dk. Mghwira alisema wahalifu hao baada ya kutekeleza nia hiyo ovu,
waliacha katika eneo la tukio kibiriti na kipande cha msokoto wa bangi.

Alipoulizwa kama nyaraka zilizounguzwa ni zinazohusiana na masuala ya
uchaguzi, Mkuu huyo wa Mkoa alisema nyaraka nyingi zilizoteketea ni za
masuala ya afya.

Alizitaja baadhi ya nyaraka zilizokuwa karibu na dirisha ambalo lilianza
kuteketea kwa moto kuwa zinazohusiana na zoezi la chanjo ya rubella,
surua na polio, iliyofanyika hivi karibuni.