Na Abel Paul, Jeshi la Polisi Mkoa Arusha
Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha limekamata watuhumiwa 702 wakituhumiwa kufanya vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa watoto na wanawake.
Hayo yameelezwa na Afisa mnadhimu namba moja wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha ACP Marry Kipesha leo December 14 katika kilele cha siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia.
ACP Mary amesema katika kipindi cha miezi ya Oktoba na Novemba 2021 kesi zilizoripotiwa kwenye vituo vya Polisi za Wilaya zote za Mkoa wa Arusha ni 693.
” Katika kipindi hicho watuhumiwa waliokamatwa ni 702 ambapo wanaume ni 419 na wanawake ni 283 wote wakituhumiwa katika makosa yanayohusu ukatili wa kijinsia,”amesema.
Amesema katika kipindi hicho cha miezi miwili jumla ya kesi ambazo zimeshinda mahakamani ni 54 na watuhumiwa 284 walikutwa na hatia ambapo wanaume ni 206 na wanawake 78 na wote wamehukumiwa vifungo mbalimbali kila mmoja kutokana na makosa yaliyowatia hatiani.
Pia amesema Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha kupitia dawati la jinsia na watoto Mkoani hapa kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za serikali na za kiraia limeendelea kutoa elimu kwa makundi yote juu ya ukatili wa kijinsia na kuzitaja taasisi inayoshirikiana nazo ni pamoja na HAKI KAZI CATALYST, CWCD, TCYLO, FAE, AVUREFA, PWC, PINGO FORUM.
Amesema licha ya kuwepo kwa changamoto kwa baadhi ya jamii kutotoa ushirikiano wa utoaji wa taarifa za ukatili wa kijinsia na watoto katika maeneo yao, Jeshi la Polisi limeendelea kutoa elimu kwa jamii na makundi yote na hivi sasa matokeo chanya ya mabadiliko hayo yameanza kuonekana.
Amesema matokeo ya elimu inayotolewa ni kupelekea kuongezeka kuripotiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia na watoto katika madawati yalipo katika vituo vya Polisi Mkoa wa Arusha.
Wakati huo huo ACP Mary amefungua dawati la Jinsia na watoto katika wilaya ya kipolisi murieti iliyopo katika Jiji la Arusha ambapo amesema kwa kitendo hicho kesi zote za ukatili wa kijinsia zitasikilizwa kwa umakini mkubwa
ACP Mary ametoa wito kwa makundi yote na taasisi za serikali, kidini na zisizo za kidini kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa Elimu dhidi ya ukatili wa kijinsia na watoto.