Wauguzi na wakunga watakiwa kutumia utaalamu wao kwa ajili ya ustawi wa taifap

WAMJW-Dodoma
Wauguzi na Wakunga nchini wametakiwa kutoa huduma kwa kuzingatia miongozo iliyopo wakati wakitoa huduma kwa weledi ili kufikia malengo na matumaini ya wateja kwa ajili ya ustawi wa Taifa.
Rai hiyo imetolewa leo na Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto – Idara Kuu ya Afya Bw. Edward Mbanga wakati wa ufunguzi wa  kikao kazi  cha kuwajengea uwezo wa kusimamia maadili na utendaji kazi wauguzi wakuu wa wilaya kinachofanyika jijini Dodoma.
Bw. Mbanga amesema  kuwa wauguzi na wakunga ndio watendaji wakuu katika vituo vya afya kwenye ngazi ya jamii hadi Taifa hivyo uwajibikaji mzuri na utawala bora utaboresha utendaji hali itayosaidia kufikia malengo mbalimbali waliyojiwekea katika ngazi zote.
“Viongozi mnatakiwa kuwa wabunifu, wachapa kazi, wenye nidhamu na mfano bora wa kuigwa katika utekelezaji wa majukumu yenu,kwahiyo  ni lazima msimamie utoaji wa huduma uliyo mzuri na wenye heshima na utu.”Alisema
Aidha, Kaimu Katibu Mkuu huyo aliwakumbusha  washiriki hao kuwa, suala la huduma za uuguzi na ukunga ni suala la  ubinadamu zaidi na kuvaa viatu vya wagonjwa wao.
“Hakuna aliyegongwa muhuri wa kuugua  au kuwa mgonjwa akalazwa ,sisi sote ni wagonjwa watarajiwa kwahiyo kama ambavyo sisi tungependa kuuguzwa vizuri, kijibiwa kwa kauli nzuri basi tuhakikishe tunasimamia maadaili ya kazi”.Alisisitiza Mbanga.
Hatahivyo alisema kuwa, Serikali inawahakikishia itaendelea kufanya kazi pamoja na waauguzi  kwa kutoa miongozo thabiti na kuhakikisha upatikanaji wa nyenzo muhimu katika hospitali na vituo vya kutolea huduma ya afya na kuboresha mazingira ya kazi yaliyo bora na salama.
Aliendelea kusema kuwa, hivi karibuni kumekuwa na malalamko  mbalimbali ya kiutendaji  na kitaaluma kutoka kwa wateja  wanaofika kupata huduma za afya na hivyo kuleta taswira mbaya  kwa taaluma yao na kuonyesha hakuna usimamizi mzuri wa utoaji huduma za uuguzi na ukunga.
“Tungependa  wateja wetu watoe sifa  badala ya malalamiko hivyo kikao hiki mje na mipango ya kuondokana na malalamiko kwani taaluma yenu ni zaidi taaluma.” alisema. 
Hata hivyo, amewakumbusha  viongozi hao kuwa mstari wa mbele kupambana dhidi  ya rushwa na kuhakikisha inatokomezwa katika maeneo yao ya kazi kwani rushwa imekuwa ikilalamikiwa na kuripotiwa katika kada ya afya nchini.