Waunga mkono msaada wa serikali wa mil60 kwa kuchimba msingi wa vyumba vitatu vya madarasa

 Na Mapuli Misalaba, Shinyanga

Wananchi wa kata ya Ibinzamata katika Manispaa ya Shinyanga wakiwemo wazazi na walezi wa wanafunzi wanaosoma katika shule ya sekondari Ibinzamata wameipongeza serikali kwa kutoa fedha shilingi Millioni 60 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa.

Wameyasema hayo leo wakati wakishiriki kuchimba msingi kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa shuleni hapo ikiwa ni hatua ya kuunga mkono juhudi za serikali, ambapo wamesema mpango wa serikali kutoa fedha hizo umelenga kuwawezesha watoto kusoma katika mazingira rafiki. 

Diwani wa kata ya Ibinzamata Ezekiel John Sabo amewapongeza wananchi wa kata hiyo kwa kujitokeza ambapo amewaomba kuendelea na ushirikiano ili kuipeleka haraka shughuli hiyo  ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 

Sabo ameihakikishia serikali kuwa pesa hiyo waliyopatiwa kwa ajili ya ujenzi wa madarasa ataisimamia vizuri ili malengo yaliyokusudiwa yaweze  kukamilika kikamilifu 

“Ninaimani kubwa sana hii shughuli tutaipeleka haraka iwezekenavyo kama yeye Rais  Samia Suluhu Hassan alivyoagiza hatutapenda tuwenyuma tunataka sisi tuwe wa kwanza kukamilisha ujenzi wa madarasa haya tunamshukuru Rais ameweka fedha na sisi wananchi tutaendelea kumpa ushirikiano kwa kutoa nguvu kazi na tunachotaka kumhakikishia kwamba pesa hii tutaisimamia vizuri ili malengo yaliyokusudiwa yaweze kukamilika kikamilifu”

Kwa upande wake mkuu wa shule ya sekondari Ibinzamata Mwalimu Kisandu Seni amesema shule hiyo imepatiwa kiasi cha shilingi milioni 60 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa hali itakayosaidia kuweka mazingira bora ya walimu kufundishia na wanafunzi kujifunzia ili kuchochea kiwango cha ufaulu  

Mkuu huyo wa shule ya Ibinzamata amesema shule hiyo inajumla ya wanafunzi 741 ambapo shule hiyo inauhitaji wa vyumba vya madarasa 6 huku vyumba 3 vimepunguzwa kupitia mpango wa serikali 

Mtendaji wa kata ya Ibinzamata mahali ilipo shule hiyo Victor Kajuna naye ameahidi kusimamia utekelezaji wa mradi huo ili fedha hivyo ifanyekazi ilivyotarajiwa 

“Na mimi niwahakikishia kwamba ile fedha milioni 60 iliyoingia itasimamiwa na kuhakikisha kila senti inafanya kazi kama ilivyotarajiwa na serikali”

Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga Jomaary Satura amesema halmashauri hiyo imepokea fedha kutoka serikali kuu kiasi cha Shilingi Millioni 880  chini ya mpango UVIKO 19 ,ambazo zimelenga kuwezesha wanafunzi wote wa kidato cha kwanza kwa mwaka wa masomo 2022 kujiunga na kidato cha kwanza kwa wakati mmoja,badala ya awamu mbili.