Na Seif Mangwangi, Arusha
Wazazi na walezi wa wanafunzi wanaohitimu darasa la saba wameshauriwa kupeleka watoto wao kwenye mafunzo ya awali ya kidato cha kwanza (Pre-form one), ili kuwaepusha na makundi ya mtaani ambayo ni hatari.
Wahitimu wa darasa la saba wakiwa kwenye mavazi rasmi yaliyobuniwa shuleni hapo |
Akizungumza kwenye mahafali ya kwanza ya shule ya msingi Shining star, Afisa Elimu Msingi Wilaya ya Arumeru, Hussein Mgawe amesema elimu ambayo watoto wameipata ni vizuri wakaiendeleza kabla hawajasahau.
“Nawashauri wazazi pelekeni watoto shule ili waweze kuwa tegemeo lenu hapo baadae. elimu sio mpaka kupata ajira, itakiwezesha kupata ujuzi wa ziada, pia wapelekeni pre form one ili kuwajengea uwezo wanapoanza rasmi kidato cha kwanza mwakani,”amesema.
Pia amesema kuna faida nyingi za watoto kusoma ikiwemo kupata ajira na kwamba ajira sio mpaka uende serikalini hata huko mtaani kuna pesa nyingi na kuwazidi hata wanaoajiriwa serikalini.
“Unachotakiwa kujua ni kwamba mtu yoyote ambaye hajapata elimu hawezi kuwa na ujuzi huko mtaani kama aliyepata elimu, kwa hiyo tupeleke watoto shuleni,”amesema.
Amesema katika mitihani ya Mock ya darasa la saba na la nne, shule ya msingi, shining star iliweza kufanya vizuri sana na kuzidi shule zingine nyingi hivyo anatumaini katika mtihani wa mwisho wa darasa la saba itashika nafasi ya juu zaidi kitaifa.
Afsa Elimu Hussein Mgawe mwenye tai nyekundu akiwa katika picha ya pamoja na wanafunzi wa jamii ya kifugaji wanasoma shuleni hapo |
“Napenda kutoa wito kwa wanafunzi wanaobaki kuendelea kujisomea mambo yote yanayofundishwa lakini na wazazi mjitahidi kusaidia hawa watoto wetu katika malezi ili kuweza kufaulu na kushika nafasi za juu kitaifa,” amesema.<
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa Shule ya Msingi Shining Star, Lomnyak Pipiyo shule hiyo ilianzishwa mwaka 2015 ina wanafunzi zaidi 300 kuanzia na chekechea hadi darasa la saba.