Mkurugenzi uzalishaji kiwanda cha AtoZ Binesh Haria akimweleza Naibu Waziri Khamisi Hamza namna mfumo wa maji taka unachakatwa kiwandani hapo |
Na Seif Mangwangi, Arusha
Serikali imekipongeza kiwanda cha AtoZ kilichopo nje kidogo ya Jiji la Arusha kwa maamuzi yake ya kujenga mtambo mpya wa kuchakata mfumo wa maji taka kiwandani hapo na kujali afya za wananchi wanaozunguka kiwanda hicho pamoja na wafanyakazi wake.
Akizungumza katika ziara aliyoifanya kiwandani hapo jana, mbele ya wataalam wa mazingira kutoka Jiji la Arusha, Halmashauri ya Arusha na NEMC, Naibu Waziri ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Khamisi Hamza amesema Atoz imefanya jambo jema ambalo viwanda vingine vinatakiwa kuiga.
Amesema amefurahi kuona agizo ambalo serikali ililitoa kwa kiwanda hicho kuhusu kuongeza ukubwa wa mtambo wa kuchakata maji taka kiwandani hapo limetekelezwa na kwamba hivi sasa maji yatakuwa salama zaidi tofauti na hapo awali.
“Kwa namna nilivyopata taarifa na baada ya kufika hapa nimeona vitu viwili tofauti, nilijua nakuja kufunga kiwanda lakini imekuwa tofauti, hongereni sana AtoZ kwa kujali mazingira na afya za watu, lakini pia nimefurahi kwamba mnawapa wafanyakazi wenu maziwa hongereni sana, sasa nataka kujua huu mradi utakamilika lini,” alipongeza na kuhoji.
Akijibu swali hilo Mkurugenzi Uzalishaji kiwandani hapo Binesh Haria amesema mtambo huo ambao umegharimu zaidi ya Bilioni1 umeshafikia hatua ya asilimia 95 kukamilika na kwamba baada ya miezi miwili utakuwa umekamilika kabisa na kuanza kutumika.
“Mheshimiwa Waziri,hadi Disemba tutakuwa tumekamilisha ujenzi wa miradi huu na kuanza kutumika lakini hadi sasa umeshaanza majaribio, tunachokiomba ni serikali kuongea na mamlaka ya maji safi na taka Arusha (Auwsa), waweze kukamilisha bomba la maji taka ili na sisi tuweze kuunganisha maji yetu sababu hilo ndio lengo kuu,”alisema.
Kufuatia ahadi hiyo ya kukamilika kwa ujenzi huo, Naibu Waziri Khamisi Hamza amewaagiza maofisa mazingira katika Halmashauri za Arusha, Jiji na Nemc kushirikiana na kiwanda cha Atoz kuhakikisha mradi huo unakamilika vizuri na kuanza kufanya kazi huku akitoa wito kwa Auwsa kukamilisha kwa wakati bomba la maji taka linalokuja kiwandani hapo.
Amesema kiwanda cha Atoz ni miongoni mwa viwanda vikubwa ukanda wa Afrika na vimekuwa vikichangia pato kubwa kwa Serikali ikiwemo kutoa ajira nyingi kwa vijana na wanawake hivyo Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan inaujali na kuthamini mchango wake.
Hata hivyo amesema pamoja na mchango huo, bado afya za wananchi wanaozunguka viwanda kama hivyo ni muhimu kuzingatiwa na ndio sababu kila mara serikali imekuwa ikifanya ukaguzi.
Mkurugenzi Uzalishaji wa Atoz Binesh Haria akiwa na Naibu Waziri Khamisi Hamza juu ya mtambo mpya wa kuchakata maji taka |
Ameutaka uongozi wa kiwanda hicho kuongeza misaada yake kwa wananchi katika ujenzi wa miradi ya kijamii ili na wenyewe wafurahie uwepo wa kiwanda hicho mbali na ajira wanazozipata.
Awali akitoa taarifa ya kiwanda, Meneja usafirishaji bidhaa nje ya nchi kiwandani hapo Sylvesta Kazi amesema kiwanda cha AtoZ kimekuwa kikitoa mchango mkubwa kwa Serikali ikiwemo ajira ya zaidi ya watu 8000 huku ikilipa kodi ya zaidi ya Bilioni17 kwa mwaka.
Mhandisi Harrison Rwehumbiza akimuonesha Naibu Waziri Hamadi Chande mtambo mpya wa kuchakata maji taka |
Kwa upande wake Meneja usalama na mazingira kiwandani hapo Harrison Rwehumbiza alimweleza Waziri kuwa mfo wa maji kiwandani hapo umekuwa ukifanyiwa ukaguzi wa mara kwa mara na mamlaka za Serikali hivyo ni vigumu kutiririsha maji machafu.
Amesema kiwanda hicho kimekuwa kikizalisha bidhaa mbalimbali ikiwemo nguo, vifungashio, chandarua chenye dawa, bidhaa za kilimo kama green house, bidhaa za plastic kama viti,meza vyombo vya nyumbani na imekuwa ikiuza bidhaa hizo ndani ya nchi na zingine kusafirisha ukanda wa nchi za SADC, Marekani na ulaya.