Waziri biteko afata nyayo za rais, atoa ya moyoni kwa wachimbaji, siwezi kuwa na amani moyoni huku mnalia




Na Mwandishi wetu, APCBLOG, Nanyumbu Mtwara.

WAZIRI wa Madini Dotto Biteko ametanabaisha kwamba katika maisha yake siku zote amekuwa akisononeshwa na kukosa amani moyoni kwa kuona  wananchi  wanyonge wanalia na kunyanyasika kwa kukosa  maeneo ya kuchimba na kulilia  leseni baada ya kunyanyaswa na mwekezaji au mtu yoyote ambaye amekuwa akifanya hivyo.

Akizungumza na wananchi wa kata ya Michiga wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara kwenye mkutano wa hadhara kufuatia ziara yake wilayani humo kukagua shughuli mbalimbali za sekta ya madini Waziri Biteko amesema suala la wananchi kunyanyasika wakati rasilimali zimewazunguka limekuwa likimkosesha amani.

Katika ziara yake katika mikoa ya Lindi na Mtwara Biteko amekutana na kilio cha wananchi karibu kila mahali kukosa maeneo ya kuchimba madini huku raslimali hizo zikiwa zimewazunguka.

“Mhe. Waziri kuja kwako leo tunakushukuru sana, Baba
kiliochetu sisi ni eneo la kuchimba, tafadhali chondee tunaomba turuhusu tukachimbe, tupate riziki, pale palipo fungiwa hata sisi tunaathirika kwa sababu palikuwa panatusaidia” alisema Mzee Faya Bozani Mussa  alipopata fursa ya kuongea mbele ya waziri Biteko.

Kufuatia kilio hicho akiwaangalia kwa huruma na kwa kuonyesha kuguswa na wananchi hao waziri Biteko litoa kauli ya kuwapatia wananchi eneo la kuchimba madini na kusababisha furaha kubwa kutoka kwa wananchi hao.

“Ndugu zangu, poleni sana, naumia sana moyoni kuwaona mnasononeka moyoni kwa ajili ya raslimali zinazo wazunguka. Rais wetu Dkt. John Magufuli anawapenda sana na mimi ameniteuwa kumsaidia lakini kazi yangu aliyo nituma ni kuja kutatua kero za wananchi katika sekta ya madini na ndio maana nipo hapa Michiga siku ya leo.”

“Mimi ni mtumishi wenu, nipo hapa kuwatumikia sipo tayari kuondoka hapa huku bado machozi yakiwa yanaendelea kutiririka. Sasa nisikilizeni. Moja, naagiza Tume ya Madini ifikapo ijumaa ijayo tarehe 16/08/2019 leseni ya lile eneo iwe imeshafika kwa Mkuu wa Wilaya ili yeye na afisa Madini Mkazi Mkoa wa Mtwara waje wakabidhi hiyo leseni.”

Aliongeza: safari yangu nimeambatana na Mkurugenzi Ukaguzi Migodi na Mazingira kutoka Tume ya Madini Dkt. Abdulrahman Mwanga yule pale, yeye atabaki hapa hataondoka japo kesho ilibidi aondoke kwa ajili ya majukumu mengine lakini hataondoka ili yule mwekezaji wenu Arafati Mrope  amsaidie kuandaa mpango kazi wa lile eneo ili ikifika leseni kazi ianze. Dkt. Utabaki hapa” alisema Biteko.
 
Maelezo hayo yaliibua shangwe, vigelegele, nderemo na vifijo kwa Wanamichiga na kusahau kilio chao.

Kufuatia kauli hiyo Mwenyeji wa eneo hilo (Chief) Njawala alisimama na kuishukuru serikali na kuipongeza huku akisema kauli ya waziri imeondoa minong’ono iliyokuwa imetanda ikiwatuhumu viongozi wa ngazi mbalimbali kuwa ndio waliokuwa wanawazuia wasichimbe wakati taratibu za kuchimba zilikuwa hazijazingatiwa.

“Waziri Mimi ni Chief wa eneo hili, nakushukuru kwa kutatua tatizo hili na umeleta amani maana awali viongozi mbalimbali ndio walio kuwa wanatuhumiwa kwamba ndio wanaozuia, binafsi nakushukuru sana” alisema Chief Njalawa.

Eneo la  Michiga limezungukwa na madini ya Chuma eneo ambalo lilikuwa limechukuliwa na mwekezaji Arafati Omari Mrope aliekuwa anachimba na kununua madini hayo kutoka kwa wananchi na baadae eneo hilo kuzuiwa na serikali kwa kuwa waliokuwa wanafanya shuguli hizo walikuwa wanafanya kinyume cha sheria.

Kwa upande mwingine Waziri Biteko alimshukuru na kumpongeza mwekezaji Arafati kwa kuwa na utii kwa serikali kwani hata alipo simamishwa asiendelee na kazi ya uchimbaji wa madini hayo mpaka afuate utaratibu alikubali na hakuendelea huku akilipa madeni ya zaidi ya Tsh. 35,000,000/= kwa wananchi waliokuwa wanachimba mchanga wa madini ya Chuma na kumuuzia mwekezaji huyo.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu Moses Machali alimshukuru Waziri wa Madini Doto Biteko kwa kufanya ziara hiyo na kutatua kero hiyo papo hapo bila kusubiri.

“Mhe. Waziri nakushukuru sana kwa ujio wako, na maamuzi ya papo kwa papo na hiyo ndio speed ya serikali ya awamu ya tano katika kutatua kero za wananchi hasa katika kufanya maamuzi yanayogusa maisha ya wananchi  wetu moja kwa moja” alise Machali.