Waziri dkt. kalemani atoa siku 9 transfoma za mradi wa jnhpp kutolewa bandarini na kufikishwa site.

 Na Mwandishi Wetu.

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani leo Julai 04, 2021 amefanya ziara ya kushtukiza katika Bandari ya Dar es Salaam kwa lengo la kujiridhisha kuhusu mchakato wa kuondoa na kusafirisha transfoma sita zilizowasili kwa ajili ya kutumika katika Mradi Mkubwa wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP).



Akizungumza na wanaandishi wa habari mara baada ya kutembelea eneo lililohifadhiwa transfoma hizo, Waziri Dkt. Kalemani amesema transfoma ambazo zimewasili nchini idadi yake ni sita kati ya transfoma zote 27 ambazo zitakazotumika katika Mradi wa JNHPP na nyingine zilizobaki zitakuja kwa mujibu wa mkataba kwa miezi tofauti ambapo hadi kufikia mwezi Septemba mwaka huu, transfoma zote zitakuwa zimeshawasili.



“Tayari transfoma 6 kati ya transfoma 27 kwa ajili ya mradi wa umeme wa Mwl. Julius Nyerere zimeshawasili, zingine 6  zitafika Julai 15, 2021 na Agosti 15, 2021 tunategemea nyingine na zitakazobaki kufikia Septemba 15, 2021 zitakuwa zimefika” alisema Dkt. Kalemani na kuongeza 



“Transfoma zinapofika bandarini sio mizigo inayopaswa kuendelea kukaa, iende site. Hivyo naagiza transfoma zote sita zilizopo bandarini, zitolewe ifikapo Julai 12, 2021. Ikumbukwe kuwa Juni 14,2022 mradi wa Julius Nyerere unapaswa kukamilika na kuwashwa, sisi tunapaswa kumsaidia Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ili aweze kutimiza ndoto za Watanzania kupitia mradi wa Mwl. Julius Nyerere. 


Dkt. Kalemani ametumia fursa, hiyo kuwataka wataalamu wote wa Sekta ya Nishati kuanza kufanya maandalizi ya kutoa vifaa na mashine muhimu mapema ili pindi vinapowasili visichukue muda mrefu na kukwamisha utekelezaji wa miradi mbalimbali.


Akizungumzia maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa JNHPP, Waziri Dkt. Kalemani  amebainisha kuwa, kuanzia mwezi Desemba, mwaka huu mitambo tisa ya kufua umeme (turbines) kwa ajili ya mradi huo itawasili nchini  huku kila mtambo mmoja ukiwa na uwezo wa kuzalisha Megawati 235.


Dkt. Kalemani ameongeza kuwa, ifikapo mwezi Mei mwakani (2022) utakuwa ni mwezi wa kufanya majaribio, matayarisho na matengenezo ya kufunga mitambo hiyo kabla ya kuwashwa rasmi kwa umeme unaotokana na mradi wa JNHPP, ambapo utawashwa rasmi mwezi Juni.


Katika kuhakikisha ubora mitambo na vifaa vinavyotumika katika Mradi wa JNHPP unazingatiwa, Waziri Dkt. Kalemani amesema, ameshatuma timu ya wataalamu kwenda kwenye nchi ambazo mitambo na transfoma zinapotengenezwa kwa lengo la kujiridhisha kuhusu viwango vya ubora vinazinagatiwa lakini uwezo wa utengenezaji wa vifaa hivyo na kuvikamilisha kwa wakati upo.


“Kwa kuwa mitambo ya kuzalisha umeme (turbines) na transfoma kwa ajili ya mradi wa JNHPP inatoka nje, tulichokifanya ni kujiridhisha, ambapo tumetuma wataalamu wetu kwenda huko kujiridhisha kama zinatengenezwa kwa viwango na je mahitaji yetu yatakamilishwa kwa wakati” alisisitiza Dkt. Kalemani


Katika ziara hiyo, Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani aliambatana na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Kheri Mahimbali, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Dkt. Tito Mwinuka, mkandarasi kampuni Arab Contractors pamoja na Maafisa kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA).