Waziri lugola awataka maafisa uhamiaji kuepuka rushwa na kutonyanyasa wawekezaji nchini

Na Felix Mwagara, Moshi (MOHA).
WAZIRI
wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, amewataka Maafisa Uhamiaji
nchini, kuepuka rushwa na kutokuwanyanyasa wageni na hasa wawekezaji
nchini.


Akizungumza
katika kikao cha Maafisa Uhamiaji Waandamizi kilichofanyika katika
Ukumbi wa Chuo cha Uhamiaji (Trita), Mjini Moshi, leo, Lugola alisema
wawekezaji ni watu muhimu katika maendeleo ya nchi, hivyo
wanaposumbuliwa kwa kunyanyaswa bila sababu za msingi ni kuvunja misingi
ya uadalifu.

Pia
Waziri Lugola aliwataka maafisa hao waache kutoa PI (tangazo la
kuondolewa mtu asiye raia nchini) zenye utata kwa maslahi binafsi bila
kuzingatia athari ambazo nchi inazipata.

“Yapo
malalamiko kwamba kuna wageni wanaingia nchini na kuwekeza kwa ubia na
Watanzania, biashara inapokuwa inaendelea Watanzania huwazunguka wageni
na kuwatengeneza mazingira ya kuwafukuza ili wapate fursa ya kumiliki
hizo biashara na hapo ndipo Idara ya Uhamiaji hutumika, acheni hayo
mambo kwa kuwa yanatuchafua kama taifa letu,” alisema Lugola.

Aliongeza
kuwa, Rais John Magufuli anatafuta wawekezaji kwa nguvu na
kuwahakikishia usalama wao na biashara zao lakini baadhi ya watumishi wa
umma badala ya kusaidia jitihada hizi wao wanatumika kuwafukuza kwa
dhuluma.

Alisema
wageni hao wakishafukuzwa na wanaacha uwekezaji wao nchini ambao
wanadhulumiwa huko waliko wanaisema nchi vibaya na kwa uzoefu huo wageni
wengine hawawezi kuja nchini.

“Tujitathimini,
tuzingatie sheria, kanuni, taratibu na miongozo yetu kwa kuzingatia
maslahi ya taifa, pia nawasihi sana mumsaidie mheshimiwa Rais kutimiza
ahadi zake kwa Watanzania ambazo amezitoa kupitia Ilani ya CCM ya
Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015 na ahadi zake nyingine mbalimbali ambazo
amekuwa akiahidi na kuzitekeleza,” alisema Lugola.

Aidha,
Waziri Lugola kabla ya kukifungua kikao hicho kilichojumuisha Maafisa
kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, alisema kikao hicho kitakuwa chachu ya
kudumisha maadili ya kazi, nidhamu, utii, na ushirikiano katika maeneo
yao ya kazi ili kwenda sambamba na kauli mbiu ya Idara hiyo ya Upendo,
Mshikamano, Uwajibikaji na Kukataa Rushwa.

“Ni
imani yangu kuwa, mtaendelea kutekeleza majukumu yenu kwa kuzingatia
Sheria, kanuni na miongozo ya utumishi wa umma katika utoaji wa huduma
bora kwa Wananchi,” alisema Lugola.

Kwa
upande wake, Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dkt. Anna Makakala, alisema
kikao hicho zitatolewa mada mbalimbali zitakazowasilishwa kuhusu rushwa
na Kanuni za Uendeshaji za Uhamiaji za Mwaka 2018 ambazo ndio mwongozo
wa utendaji kazi wa  Idara ya Uhamiaji.

“Kwa
kuwa Idara yetu ya Uhamiaji inatoa huduma mbalimbali kwa wananchi
ikiwemo pasipoti, vibali vya ukaazi, pasi pamoja na viza, hivyo kupitia
kikao hiki tutazingatia kikamilifu mada hizo kwa kuwa zitatusaidia
katika kutoa huduma bora kwa maslahi ya Idara yetu, Wizara na taifa kwa
ujumla,” alisema Dkt. Makakala.