Waziri nape azindua shahada mpya ya habari uhasibu

 Na Seif Mangwangi, Arusha

Chuo Cha Uhasibu Arusha ( IAA), kimeanzisha kozi mpya ya shahada ya Media Anuai na Mawasiliano kwa Umma (Multi Media and Mass Communication),  na kuwa chuo cha kwanza nchini kutoa shahada hiyo.

Akizungumza kwenye uzinduzi wa shahada hiyo Jana Julai20,2023, Chuoni hapo Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye, amesema kozi hiyo imekuja wakati muafaka huku Serikali ikiwa imepitisha mabadiliko ya sheria ya huduma za habari.

Amesema uzalishaji na ulaji wa maudhui ya vyombo vya habari pamoja na mitandao ya kijamii katika kipindi hiki cha Maendeleo ya Sayansi na Teknolojia unategemea sana Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).

“TEHAMA ndio msingi wa Media Anuwai, hivyo uamuzi wa Chuo Cha Uhasibu Arusha kuamua kuanzisha shahada hii kwa kuunganisha Media Anuwai na Mawasiliano kwa Umma ni uamuzi sahihi na kwa takwimu nilizo nazo hiki ndio chuo Cha kwanza kutoa shahada hiyo nchini,”amesema Waziri Nape.

Waziri Nape amesema Tasnia ya Habari na Mawasiliano inahitaji watu mahiri wenye weledi watakao kuwa daraja la kuunganisha jamii na Serikali na hivyo kutoa wito kwa Watanzania kujiunga na chuo hicho ili kupata taaluma hiyo muhimu.

” Vyombo vya habari dhabiti hutathmini, huchanganua na kuanzisha mijadala inayochochea kupatikana kwa utatuzi wa changamoto mbalimbali za jamii na utambulisho chanya wa nchi Kimataifa,”amesema.

Aidha  Waziri Nape ametoa rai kwa wamiliki wa vyombo vya habari Mkoa wa Arusha kutoa fursa kwa wanafunzi watakaosoma shahada hiyo Chuoni hapo kupata nafasi ya mazoezi ya vitendo ili kuwajengea uwezo wa namna vyombo vya habari vinafanyakazi na kupata uzoefu.

Mkuu wa Chuo Cha Uhasibu, Profesa  Eliamani Sedoyeka amesema chuo hicho kimeamua kuanzisha shahada hiyo baada ya kufanya utafiti na kugundua uwepo wa hitaji la wataalamu wa media Anuai na Mawasiliano kwa umma nchini.

Amesema chuo kimeshajipanga kuanza kupokea wanafunzi wa mwaka wa kwanza na kwamba miundo mbinu yote iko tayari ikiwemo studio ya kisasa ya kutolea mafunzo pamoja na wakufunzi wa kutosha.