Doreen Aloyce, Dodoma
KATIKA Juhudi za kuendeleza uchumi wa Viwanda hapa nchini,Wizara ya Uwekezaji,Viwanda na Biashara imeandaa mafunzo maalumu ya KAIZEN kwa watumishi wa Wizara hiyo lengo likiwa ni kuboresha utendaji kazi katika maeneo ya kazi na kuleta ufanisi mkubwa.
Aidha mafunzo hayo yenye kauli mbiu ” KAIZEN kwa Tanzania ya viwanda shindani na maendeleo shirikishi” yamelenga pia watumishi waliohamia Wizara ya Uwekezaji na wengine ambao hawakuwahi kupata mafunzo hayo.
Akifungua mafunzo hayo ya siku tatu, Kaimu Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu (DAHRM) kutoka Wizara ya Uwekezaji,Viwanda na Biashara Bi Veronica Nchango amewataka washiriki kuwa Chachu kuchangia kukuza maendeleo ya viwanda na kuongeza uchumi wa Nchi.
Amesema Serikali inategemea kupata matokeo yenye tija kupitia mafunzo hayo huku akiwataka wakufunzi kuwafatilia kwa ukaribu ambao wamepata elimu kujua kama wanayofundishwa wanayafanyia kazi ili kuleta tija kwa Taifa letu na sio kuishia Kutoa mafunzo pekee.
“Niwashukuru wale waliowezesha mafunzo haya wakiwemo Jaica ambao wamefadhili mradi huu ambao unalenga kuongeza tija na ubora Katika Sekta zote hivyo niwaombe muwe wasikivu kwa siku hizi tatu mkitoka hapa muwe mmeiva “
“Tunapaswa kuwa kioo kupitia KAIZEN kuwa na mtazamo chanya ili Jamii ione matokeo ya kuendeleza maendeleo ya viwanda hapa nchini” amesema Mchango.
Janne Lyatuu Mkuu wa Kitengo cha KAIZEN Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Janne Lyatuu ametumia fursa hiyo kuiomba Wizara kuwa mafunzo hayo yawe endelevu Nchi nzima.
“Tunaomba mafunzo yawe endelevu kwa watumishi wa Wizara na Nchi nzima na niwaombe wale wenye muamko wa kusoma masomo haya waelekee kwenye kuleta Mabadiliko kwa wizara.
Kwa upande wake Meneja wa Dodoma Semphao Manongi amesema kuwa endapo wataitumia dhana ya Kaizeni itasaidia kubadilisha uchumi wa nchi .
“Endapo tukiifanyia kazi hii dhana na kuitekeleza kama inavyotakiwa tunaweza kufufua viwanda vyetu na kuliokoa Taifa letu ” amesema Manongi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti washiriki wa mafunzo hayo wamesema kuwa mafunzo hayo yataenda kuwajenga na kuwaongezea uelewa ambao utawasaidia kuinua uchumi wa Nchi kupitia viwanda.