Kiongozi wa timu ya zoezi la kuandika anwani za makazi katika ya Kaloleni Erinesta Moshi,(aliyevaa kofia), akiwasiliana jambo na timu yake inayofanyakazi hiyo katika kata ya kaloleni |
Na Seif Mangwangi,Arusha
Zoezi la kuweka majina ya mitaa na namba za anwani za makazi limeanza rasmi leo katika kata tano za Jiji la Arusha huku sehemu kubwa ya zoezi hilo likielezwa kufanyika vizuri.
kwa mujibu wa Msimamizi mkuu wa zoezi hilo kata ya Kaloleni Erinesta Moshi, ambaye ni mmoja wa maafisa mipango miji jiji la Arusha, anasema kata ya Kaloleni zoezi limeenda vizuri ijapokuwa kumekuwa na changamoto ndogo ndogo ambazo zinaendelea kupatiwa ufumbuzi.
Ametaja changamoto zilizojitokeza ni pamoja na kurudiwa kwa baadhi ya namba kwenye maeneo ambayo zimeshawekwa hapo awali na hivyo kulazimika kurudia kufuta namba mpya zilizotolewa kwa baadhi ya maeneo hayo.
“Kumejitokeza baadhi ya changamoto mfano ya baadhi ya namba kujirudia kwenye baadhi ya barabara na mitaa lakini nimejaribu kuwaelewesha vijana wangu wameelewa na wamerudia kufuta namba walizokosea na zoezi limeenda vizuri,”amesema.
kuhusu uhakiki wa majina ya mitaa na vibao Erinesta amesema zoezi hilo limeenda vizuri pia kwa kuwa timu yake yote anayofanya nayo kazi katika kata ya Kaloleni ameigawia ramani za mipango miji na kuhakiki maeneo ambayo yalishakuwa na majina.
Amesema baada ya zoezi la leo februari 15 kukamilika, timu ya wataalam wa Jiji itakutana na Mkurugenzi wa Jiji Dkt John Pima kwaajili ya kufanyia tathmini zoezi hilo na kuendelea.
Zoezi la kuweka anuani za makazi katika jiji la Arusha lilizinduliwa rasmi jana Februari 14,2022 na Mkuu wa Wilaya ya Arusha Said Mtanda ambaye katika hotuba yake aliwataka wasimamizi wa zoezi hilo kuifanya kazi hiyo kwa uadilifu wa hali ya juu kwa kuwa wameaminiwa.
Alisema kutokana na utendaji mzuri uliotukuka wa Mkurugenzi wa Jiji Dkt John Pima ana uhakika Arusha itafanya vizuri na kuzizidi Halmashauri zingine.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Jiji Dkt John Pima, zoezi hilo linafanyika katika kata tano za awali ambazo ni Kaloleni, Kati, Sekei, Themi na Levolosi ambapo zoezi la namna hilo lilishafanyika katika kata hizo hivyo kinachofanyika hivi sasa ni kuhakiki na kufanyia marekebisho madogo madogo.