Karibu kilifair 2024 kufunguliwa kesho jijini arusha.

Eneo la Kisongo lililopo Jijini Arusha ambalo Maonesho ya Karibu Kill Fair yanatarajia kufanyika.

Na Ashura Mohamed

Arusha
 Wananchi na Wadau wa Utalii wametakiwa kuchangamkia fursa ya uwepo wa maonesho ya Karibu KiliFair 2024 yanayotarajiwa kuanza Juni 7 Mwaka huu.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Paul Christian Makonda ametoa kauli hiyo leo mara baada ya kukagua maandalizi ya maonesho hayo yatakayofanyika kwenye viwanja vya Magereza Arusha na kufunguliwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki.
Mkuu wa mkoa wa Arusha Paul Makonda akizungumza na vyombo vya habari katika uwanja wa Magereza Jijini Arusha.

Maonesho hayo yanatarajiwa kushirikisha Makampuni ya Kimataifa zaidi ya 700 kutoka kwenye Mataifa takribani 50 na yakitarajia kushirikisha Makampuni wenyeji zaidi ya 500 yatakayoonesha bidhaa na kazi mbalimbali kwenye maonesho hayo.
Makonda amewataka wadau wa utalii kushiriki kikamilifu kwenye maonesho hayo ili kutangaza huduma zao pamoja na kubadilishana uzoefu na makampuni mengine ili kuweza kusaidia kukuza utalii Mkoani Arusha.
Amesema maonyesho hayo yatachochea na kusisimua Utalii wa Arusha kwa kiasi kikubwa hivyo kutoa rai Kwa wananchi na raia wote wa kigeni kushiriki kikamilifu kwani suala la ulinzi na usalama kwa mkoa wa Arusha limeimarishwa wakati wote.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kampuni ya Kili Fair Bwana Dominic Shoo amemuambia Mkuu wa Mkoa kuwa maandalizi yamekamilika kwa asilimia 95 akisisitiza kuwa maonesho ya mwaka huu yameboreshwa zaidi ikiwemo kuongeza muda wa maonesho pamoja na kutenga maeneo maalum kwa ajili ya michezo ya watoto.

Mkuu wa mkoa wa Arusha Paul Makonda akizungumza na baadhi ya wadau wa Maonyesho ya Karibu Kilifair leo Jijini Arusha.

Maonesho ya Karibu Kili Fair 2024 yanafanyika kwa awamu ya tisa Jijini Arusha likiwa ni jukwaa maalum la kuyaweka pamoja makampuni ya ndani na nje ya nchi yanayohusika na sekta ya Utalii Kwa lengo la kubadilishana bidhaa, huduma na uzoefu unaotokana na sekta ya Utalii duniani.