7 watiwa mbaroni kwa kuwaua kwa mapanga wanandoa wawili

Watu 
saba wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Kagera, wakituhumiwa
kuwaua wanandoa wawili kwa kuwakata sehemu mbalimbali za miili yao,
chanzo kikidaiwa kuwa ni mgogoro wa ardhi.


Kamanda
wa Polisi mkoani Kagera, Revocatus Malimi, aliwaambia waandishi wa
habari jana kuwa tukio hilo lilitokea Januari 14 mwaka huu saa saba
usiku katika Kijiji cha Mabale, Kata ya Nyakahura wilayani Biharamulo.

Alisema
kuwa wakati wanandoa hao wakiwa wamelala, mlango wa nyumba yao
ulivunjwa na kuvamiwa na kundi la watu ambao hawakufahamika na kuanza
kuwakata kwa kitu chenye ncha kali sehemu mbalimbali za miili yao na
kusababisha kupoteza maisha papo hapo.

Aliwataja waliouawa katika tukio hilo kuwa ni Elizeus Rubanie (35) na mke wake, Juliana Joseph (28).

“Kabla
ya tukio hilo, kulikuwa na mgogoro wa ardhi kati ya marehemu na baadhi
ya wanaukoo kwa muda mrefu, uliotokana na kuachiwa eneo alilokuwa
akiishi na babu yake, aliyehama kwa shinikizo la wanajamii waliomtuhumu
kuwa ni mwizi,” alidai.

Kamanda
Malimi alidai kuwa baada ya babu huyo kuhama na kumwachia eneo hilo
mjukuu wake, baadhi ya wanajamii waliungana na baadhi ya ndugu kwenye
ukoo huo, hasa shangazi wawili wa marehemu, na kuanza kumsakama marehemu
na familia yake na kumtolea vitisho.

Aliwataja
wanaoshikiliwa kuwa ni Sophia Joseph (45), Joseph Magambo (47),
Alphonce Karoli (37), Martine Makabe (36), Alex Leopord (44), Salvatory
Mwiliza (38) na Aloyce Leopord (45).

Kamanda
Malimi alidai upelelezi bado unaendelea ili kubaini watu wote
waliohusika na tukio hilo, na kuwa watuhumiwa watafikishwa mahakamani
wakati wowote baada ya upelelezi kukamilika.