Afisa elimu mkoa wa kigoma aonya wazazi wanaokusanya watoto na kuwatafutia walimu majumbani

Afisa Elimu Mkoa wa Kigoma Majuto Njunga akimkabidhi mwakilishi wa watoto ndoo na sabuni kwa niaba ya watoto mwenzake

Diana Rubanguka Kigoma.

Afisa elimu Mkoa wa Kigoma Majuto Njunga ametoa rai kwa wazazi wanaotengeneza makundi na kukusanya watoto kuwatafutia walimu wakuwafundisha majumbani kuacha tabia hiyo kwakuwa ni kitendo cha kukiuka agizo la serikali katika harakati za kupambana na maambukizi ya virusi vya Korona.

 Aliyasema hayo jana akimuwakilisha katibu tawala Mkoa wa Kigoma katika zoezi la kukabidhi vifaa vya kujikinga na maambukizi ya Korona vilivyolotewa na shirika la Compassion Of Africa kupitia muungano wa makanisa 12 linalohudumia watoto 2,718, wanawake wakiwa 1384 wanaume 1334 katika Manispaa ya Kigoma Ujiji.

Njunga alisema, amepata tetesi kuna kinamama wanakiuka maelekezo ya Serikali kupitia watoa huduma wa afya kwa kuunda makundi ya watoto na kuwatafutia walimu hali ambayo ni hatari kwa kuwa msongamano hautakiwi.

 Alieleza namna ambavyo nyumba binafsi hazipaswi kutumika kufundishia watoto kwa kuwa mazingira yake hayajajengwa kwa ajili ya madarasa huku akisema walimu hao hawajathibitishwa na serikali na kuwaomba kutumia Televisioni zenye vipindi vya elimu vinavyotolewa hivi sasa kwa kuwa walimu wake wameandaliwa na serikali.

 Awali akizungumza kwa niaba ya wachungaji mchungaji Riziki Jacksoni alisema, Compassion inaendelea kutoa huduma kwa watoto wakiwa majumbani hasa elimu ya kujikinga na maambukizi ya Korona kwa mujibu wa wataalamu wa afya, kugawa vyakula na kusimamia matibabu.

 Jackson alisema shirika la compassion of Afrika limefanikiwa kununua vifaa vya kujikinga na mlipuko wa korona vyenye thamani ya fedha za kitanzania shilingi milioni 45,472 ambavyo ni ndoo za ujazo wa lita kumi zenye koki pamoja na sabuni za maji kwa ajili ya kunawia mikono.

 Kwa niaba ya wazazi Malieta Alex alitoa shukrani, na kusema kuwa kulingana na hali halisi ya maisha ya wasingemudu kununua ndo na sabuni ambavyo tangu kuazna kwa mlipuko wa korona vinauzwa bei ghali.