AICC, PSSF WAINGIA MAKUBALIANO UJENZI WA UKUMBI MKUBWA WA KIMATAIFA WA KWANZA AFRIKA WA MT. KILIMANJARO NA HOTELI YA NYOTA5

  • UTAJENGWA ARUSHA, KUCHUKUA WATU 5000, KUKAMILIKA KWA MIAKA2

Na Seif Mangwangi,Arusha

KUELEKEA Mkutano Mkuu wa Dunia wa wadau wa Nyuki 2027, kituo cha mikutano cha kimataifa cha AICC na shirika la hifadhi ya jamii la PSSSF zimeingia makubaliano ya kihistoria ya ujenzi wa kituo kikubwa cha mikutano Afrika kitakachogharimu zaidi ya Dola Milioni 500 fedha ambazo ni mkopo kutoka katika shirika hilo la hifadhi ya jamii.

Mkutano mkubwa Duniani wa wadau wa nyuki unaojulikana kama Apamondia umepangwa kufanyika mwaka 2027 Nchini Tanzania ambapo zaidi ya wageni 60,000 wanatarajiwa kuhudhuria mkutano huo ambao utafanyika jijini Arusha.

Makubaliano hayo yamefanyika juzi jijini Arusha huku yakishuhudiwa na mawaziri wanne ambao ni Thabiti Kombo Waziri wa Wizara ya Mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika kimataifa, Ridhiwani Kikwete Waziri wa nchi ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na wenye ulemavu, William Lukuvi Waziri wa nchi ofisi ya Waziri Mkuu Bunge na Uratibu pamoja na Pindi Chana Waziri wa Utalii na Maliasili.

Watendaji wa Kituo cha Mikutano cha AICC Christine Mwakatobe na Abdulrazaq Abdu wa PSSSF wakibadilishana hati za makubaliano ya ujenzi wa kituo cha kimataifa cha Mt.Kilimanjaro huku mawaziri Ridhiwani Kikwete na Mahmoud Kombo wakishuhudia

Waziri Ridhiwani Kikwete mwenye dhamana ya mfuko wa hifadhi ya jamii PSSSF amesema kituo hicho kitajulikana kwa jina la Mount Kilimanjaro Convention Center kitakuwa na uwezo wa kuingiza wageni 5000 kwa mara moja na kufanya kuwa moja ya ukumbi mkubwa barani Afrika.

Amesema ujenzi huo utaenda sambamba na ujenzi wa hoteli kubwa ya nyota tano yenye uwezo wa kuchukua idadi kubwa ya wageni lengo likiwa ni kutoa fursa kwa wageni watakaohudhuria mkutano katika ukumbi huo waweze pia kupata malazi katika eneo la karibu.

Kikwete amesema ujenzi wa kituo hicho cha mikutano ni maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan pamoja na utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ambayo inaelekeza kujengwa kwa ukumbi mkubwa wa Mikutano utakaoleta Mikutano Mikubwa duniani.

“ Ninachopenda kusisitiza hapa ni kwa kila mmoja kwenda kutekeleza majukumu yake, taasisi yoyote itakayokwamisha mradi huu tutaichukulia hatua na kama kuna sehemu kutakuwa na mkwamo ni vyema tukawasiliana mapema ili tuweze kutatua na ujenzi uendelee,”amesema Kikwete.

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mahmoud Thabit Kombo amesema ujenzi wa ukumbi huo umefanyika Arusha kwa kuwa ndio eneo ambalo linafaa kufanyika kwa mikutano kwa kuwa hakuna wingi mkubwa wa magari unaoweza kusababisha foleni ya muda mrefu.

“Ndugu zagu juzi mkutano wa wakuu wa nchi uliofanyika Jijini Dar es salaam tulilazimika kufunga barabara jambo ambalo lilisababisha foleni kubwa, lakini hapa Arusha hilo ni nadra sana kutokea, na niwaeleze tu katika mkutano ule tulikataa watu zaidi ya 1800 ambao walitaka kushiriki kwa kuwa hatukuwa na ukumbi wala hoteli za kuhifadhi watu hao,”amesema Kombo.

Amesema utalii wa Mikutano umekuwa faida kubwa kwa nchi na kutoa fursa kwa wafanyabiashara, “kwa mujibu wa shirika la utalii duniani, mtu mmoja anayehudhuria mkutano kwa siku hutumia si chini ya dola 100, akikaa kwa siku tano anatumia fedha nyingi zaidi, kwa hiyo kwa hesabu za kawaida tu mkutao mmoja unaweza kuingiza zaidi ya dola milioni4, hii ni faida nzuri sana ambayo tunaenda kuipata,”amesema.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha Paul Makonda amesema kwa kuwa Jiji la Arusha limeteuliwa kuwa kituo cha mikutano nchini, atahakikisha hakutakuwa na vikwazo vyovyote vitakavyokwamisha ugeni wowote utakaokuwa ukiingia mkoani humo huku akisisitiza watanzania kuendelea na uwekezaji wa hoteli mkoani humo ili kujitosheleza kwa malazi.

“Arusha pia tunahitaji usafirishaji, SGR itakuja Arusha, tayari Arusha tuna magadi soda ambayo yanahitaji kusafirishwa lakini pia bandari ya pale Tanga ni moja ya  bandari kubwa kutokana na maboresho yanayofanywa lakini wenzetu wa nchi jirani wamegundua kusafirisha mizigo kupitia Arusha ni njia fupi sana, kwa hiyo tunasubiri tu tamko lini tunaletewa SGR,”amesema Makonda.

Katika hafla hiyo ambayo pia ilihudhuriwa na Katibu Mkuu Wizara za Mambo ya nje na ushiriano wa kimataifa pamoja na katibu mkuu wizara ya ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, vijana na wenye ulemavu, wakuu wa taasisi mbalimbali chini ya wizara hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa AICC, Christine Mwakatobe na Mkurugenzi wa Mfuko wa PSSSF Abdulrazaq Abdu waliweka saini nyaraka za makubaliano ya ujenzi wa kituo hicho.

Mawaziri Mahmoud Kombo, Pindi Chana na Ridhiwani Kikwete wakishuhudia utiaji saini wa makubaliano ya ujenzi wa kituo kikubwa cha mikutano cha Mt.Kilimanjaro