Ajinyonga kwa hasira baada ya mkewe kuuza kondoo na kutumia fedha bila kumshirikisha

Na  Rehema Matowo, Mwananchi 

 Paulo Hassan, mkazi wa kijiji cha Gamash, kata ya Bulela wilayani
Geita, anayekadiriwa kuwa na zaidi ya miaka 40 anadaiwa kujinyonga na
shuka kwa kile kinachodaiwa kuwa ni hasira baada ya mkewe kuuza kondoo
na kutumia fedha bila kumshirikisha.
Akizungumza na Mwananchi kwa simu jana, mke wa marehemu, Jenipha
Lateremla alidai kuwa mumewe alijinyonga usiku wa kuamkia Januari
18,2020 baada ya kutokea ugomvi baina yao.
Jenipha alisema usiku wa Januari 17 wakiwa chumbani, mumewe alianza
kuhoji alikopeleka kondoo, alimueleza kuwa alimuuza kwa ajili ya
maandalizi ya Sikukuu ya Krismasi na fedha hizo alizitumia kwenye
sikukuu.
“Tukiwa tumelala usiku, akaniambia tena, unajua moyo wangu ulivyo na
hasira, hela umefanyia nini nilivyoona hivyo kwa kuwa akikasirika huwa
ananipiga nilitoka nje nikamuacha,” alisema Jenipha.
Alisema alipotoka nje mumewe alifunga mlango na mkewe akabaki nje na
kuwagongea watoto na asubuhi watoto walipoamka walimgongea baba yao kwa
ajili ya kumsalimia, lakini hakuitikia na walipochungulia ndani walikuta
amejinyonga kwa shuka yake ya kulalia.
Via Mwananchi