Anaswa akijaribu kutorosha madini dodoma

Na.Faustine Gimu Galafoni.Dodoma.
MTU
mmoja Khalifa Mohamed Kinyaka (51) anashikiliwa na jeshi la Polisi
Mkoani Dodoma, kwa tuhuma za kutorosha na kusafirisha viroba sita vya
madini vyenye uzito wa kilogramu 410.75.


Kamanda
wa Polisi Mkoani Dodoma Gilles Muroto, amesema mtu huyo alikamtwa
katika basi la abiria la Jambo Express, lenye namba za usajili T 704
DLF, linalofanya safari zake kati ya Katesh na Dar es salaam.
Amesema
mbinu iliyotumiwa na mtuhumiwa ni kupanda basi tofauti na lile
alilopakia viroba vingine vitano, katika basi la Emigrace lenye namba za
usajili T 730 DGL lililokuwa likiendeshwa na Adrian John Temba (32),
likitokea Babati Manyara kuelekea jijini Dar es salaam.
Hata
hivyo uchunguzi wa Jeshi la Polisi unaonesha kuwa madini hayo yametoka
katika machimbo ya Kijiji cha Yobo Kwahemu Wilayani Chamwino, na juhudi
za kuwapata washiriki na wanunuzi zinaendelea ili kuweza kuwafikisha
Mahakamani.
Akifafanua
juu ya taratibu husika za usafirishaji madini, Mhandisi Migodi wa Ofisi
ya Madini Dodoma Sasi Marwa, amesema muhusika alipaswa kuwa na vibali
toka eneo husika na kwamba tathmini itafanywa ili kujua thamani halisi
ya madini hayo.
Tukio
hili linakuja ikiwa ni muda mfupi baada ya Jeshi la Polisi Mkoani
Dodoma, kuwakamata watu zaidi ya 70 kwa  makosa mbalimbali   Septemba 21
mwa ka huu , ikiwemo usafirishaji wa mafuta ya vyombo vya moto kwa njia
hatarishi.