Mkuu
wa Wilaya ya Iringa Bw. Richard A. Kasesela akizungumza na Mkurugenzi
wa udhibiti ubora TBS Bw. Lazaro Msasalaga (wa pili kushoto), Kaimu Mkuu
wa kanda ya nyanda za juu kusini TBS Bw. Abel Mwakasonda pamona na
Mchumi kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara Bi. Chresencia Mwimbwa
walipoenda kumtembea ofisini kwake kabla ya kuanza kwa mafunzo kwa wadau
wa mafuta ya kula Iringa. Maafisa wa TBS wakitoa elimu juu ya uhifadhi na ufungashaji bora wa mafuta ya kula kwa muuzaji katika soko mkoani Iringa.
Mkuu
wa Wilaya ya Iringa Mhe. Richard A. Kasesela, ameagiza viongozi wa
Halmashauri za wilaya kuanzisha maeneo maalum ya kusindikia bidhaa ili
kuwezesha wajasiriamali wadogo kuzalisha bidhaa bora zinazokidhi matakwa
ya viwango.
Mhe.
Kasesela aliyasema hayo wakati wa akifungua rasmi mafunzo kwa wadau wa
mafuta ya kula mkoani Iringa ambapo yanategemea pia kuhusisha mikoa ya
Njombe na Mbeya.
Kwa
upande wake Mkurugenzi wa Udhibiti Ubora wa TBS Bw. Lazaro Msasalaga,
alisema kuwa ili mafuta yakidhi viwango ni lazima kufuata kanuni bora za
kilimo ikiwemo kutumia mbegu bora na kuvuna kwa wakati, kanuni bora za
usindikaji na kanuni bora za afya ikiwemo uhifadhi wa mafuta ya kula
katika eneo ambalo halipigwi na jua kwani kwa kufanya kinyume na hivyo
itasababisha kuzalishwa kwa kemikali zisizofaaa kwa binadamu katika
mafuta hayo na kusababisha madhara makubwa ikiwemo magonjwa.
Bw.
Msasalaga alisisitiza zaidi ni lazima kufuata kanuni hizo kwa pamoja na
siyo kutegemea kanuni ya eneo moja tu kwani kwa kufanya hivyo kunaweza
kusababisha bidhaaa kutokidhi matakwa ya viwango.
Naye
Kaimu Mkuu wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini wa TBS Bw. Abel Mwakasonda,
alitoa elimu kuhusu taratibu za uthibitishaji wa bidhaa na usajili wa
bidhaa na majengo ya vyakula na vipodozi ambapo aliwaasa wenye majengo
na bidhaa zote zinazotakiwa kusajiliwa wafanye hivyo haraka kabla hatua
kali za kisheria hazijachukuliwa dhidi yao.
Mafunzo
haya yamehusisha pia Taasisi mbalimbali ikiwemo SIDO, Wakala wa Vipimo,
BRELA pamoja na Maafisa Biashara, Afya na Maendeleo ya Jamii kutoka
Halmashauri husika.
TBS
tayari imekwishatoa elimu ya aina hii awamu ya kwanza katika kanda ya
kati ambayo ilihusisha wilaya zilizopo mikoa ya Dodoma, Singida na
Tabora ambapo wadau zaidi ya 1700 walifikiwa na awamu ya pili ilihusisha
mkoa wa Kigoma ambapo wakulima, wasindikaji na wauzaji zaidi ya 2000
walifikiwa.