Asilimia 40 wanawake walioajiriwa sekta ya utalii wanafanyiwa vitendo vya ukatili

Na Seif Mangwangi, Arusha
Licha ya asilimia 60 ya wanawake kuajiriwa katika sekta ya utalii nchini, asilimia 40 ya waajiriwa wanadaiwa kufanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia kupitia maeneo walipoajiriwa.

Hayo yameelezwa leo jijini hapa na Waziri wa Ulinzi na jeshi la kujenga Taifa Dkt Stegomena Tax katika hotuba yake ya ufunguzi wa kongamano la wanawake Kanda ya kaskazini linaloendelea jijini Arusha kuelekea siku ya wanawake duniani.

Dkt Tax amesema kauli mbiu ya kongamano hilo ambayo ni ushiriki wa wanawake katika utalii na maliasili kuelekea miaka 30 ya azimio la Beijing ambapo Mada kumi na saba zitajadiliwa na wataalam wabobezi ikiwemo ukatili wa wanawake sekta ya utalii.

Amesema fursa za wanawake zimezingatiwa sana nchini na zimeendelea kuimarika kupitia sekta tofauti pamoja na kuimarisha usawa wa kijinsia.

Dkt Tax ametoa wito kwa wanawake kutendea haki nafasi wanazopewa ili kuondoa dhana ya wanawake kuwa hawawezi na kuwataka wale wote wanaobeza wanawake kuwa hawawezi kuondokana na dhana hizo.

Amesema Serikali imeimarisha sheria na sera zinazolinda wanawake na kufungua fursa kwa wanawake kote nchini ikiwemo kuwapatia mikopo ya ujasiriamali.

“Sio katika sekta ya utalii tu hata sekta ya uongozi wanawake wengi wameteuliwa ikiwemo mimi kuwa waziri wa kwanza wa ulinzi na jeshi la kujenga Taifa lakini pia majaji ni wengi sana wameteuliwa,”Amesema.

Amesema baadhi ya kazi zimekuwa zikionyesha ni za wanaume kumbe sio, ” nilipoteuliwa Rais alisema uwaziri wa ulinzi sio kwenda kubeba mizigo ni kusimamia sera na sheria ambazo hata wanawake wanaweza,”amesema.

Amesema pamoja na kuendelea kupigania haki ya wanawake na mtoto wa kike tuhakikishe tunapigania haki za ustawi wa watoto wote wa kike na wa kiume sababu changamoto ni nyingi kwa watoto wa kiume pia ikiwemo kutumia dawa za kulevya, kulawitiwa na ushoga.

Dkt Tax amesema kongamano hilo litajadili athari za kijinsia tangu azimio la Beijing na kuja na mikakati ya namna ya kuendelea kukabiliana nayo.

” Kauli mbiu ya mwaka huu inasema Wanawake na wasichana 2025 tuimarishe haki,usawa na uwezeshwaji, Wanawake tunapopewa nafasi tuzitendee haki, ili kuondoa dhana ya wanawake hawawezi na wale wanaobeza wanawake hawawezi hizi ni hisia Potofu mfano ni Rais wetu ameweza kuonyesha nafasi ya wanawake,”amesema.

Kwa upande wake Naibu waziri wa wizara ya Maendeleo ya jamii, jinsia na makundi maalum, Mwanaidi Ally Khamisi amesema kupitia kampeni ya Royal Tour, kumekuwepo na ongezeko la watalii, ukuaji wa pato la taifa na pato la mmoja mmoja.

Katibu Mkuu wizara ya maendeleo ya jamii, jinsia na makundi maalum Dkt John Jingu amesema maadhimisho ya siku ya wanawake duniani mwaka huu 2025 yamepambwa na shughuli mbalimbali ikiwemo makongamano ya kuwawezesha wanawake kiuchumi.