Baba aua mtoto wa miaka mitatu kwa kumcharanga mapanga bukoba

Picha haihusiani na habari hapa chini
Na Ashura Jumapili – Malunde 1 blog Bukoba
Mwanaume aliyejulikana kwa jina la Leonard Kishenya anatuhumiwa kumuua
kikatili mtoto wake wa kambo mwenye umri wa miaka mitatu kwa
kumcharanga mapanga sehemu mbalimbali za mwili wake kisha kutenganisha
mkono wa kushoto.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 03,2020 ofisini kwake 
Kamanda wa polisi mkoa wa Kagera (ACP )Revocatus Malimi alisema tukio
hilo lilitokea Januari mosi mwaka huu ,usiku wa kuamkia mwaka mpya saa
6:40 usiku katika kijiji cha Katorerwa Wilaya ya Missenyi mkoani Kagera
ambapo mtoto Careen Crispine mwenye umri wa miaka (03) aliuawa.

Alisema marehemu alikuwa anaishi na mama yake mzazi aitwaye Domina
Andrew (30 )aliyekuwa ameolewa na Leonard Kishenya (36 ) ambaye
anatuhumiwa kwa mauaji ya mtoto huyo.
Alisema kabla ya tukio hilo la mauaji wanandoa hao walitoka kwenda
kwenye mkesha wa mwaka mpya wa 2020 walikuwa wanakunywa pombe na
walirudi nyumbani majira yasaa 6:40 usiku na walipofika kulitokea
ugomvi kati ya wanandoa hao ambao chanzo chake hakijafahamika.
Kamanda Malimi alieleza kuwa kutokana na ugomvi huo kuwa mkali, mke
aliamua kukimbia na kwenda kulala kwa jirani na kumuacha mtoto wake
ndani akiwa amelala.
Alisema Januari Mosi mwaka huu majira ya saa moja asubuhi mke alirudi
nyumbani na kushuhudia mtoto wake akiwa ameuawa kwa kukatwakatwa na
kitu chenye makali sehemu mbalimbali za mwili wake kama vile kichwani na
kuutenganisha mkono wa kushoto na mwili.
“Mwili wa mtoto huyo ulikutwa umelala kifudifudi nje ya nyumba yao
wakati alikuwa, amelala ndani. Mume ambaye ni mtuhumiwa wa tukio hilo
hakuwepo na alikuwa ametorokea kusikofahamika”,alieleza.
Alisema jeshi la polisi kwa kushirikiana na wananchi walifanikiwa
kumkamata na wanaendelea kumhoji chanzo cha kufanya mauaji ya kikatili
kwa mtoto asiyekuwa na hatia naatafikishwa mahakamani.