Babu wa loliondo aibuka na corona, aiomba serikali kupeleka wagonjwa wakapate kikombe

Mchungaji Ambilikile Mwasapile kushoto akimpatia kikombe cha dawa waziri wa Ardhi, William Lukuvi (kulia) wakati huo akiwa waziri wa nchi ofisi ya Waziri Mkuu, Bunge na Sera

Na Mwandishi Wetu
WAKATI Dunia ikiwa kwenye
taharuki kubwa ya kupambana na maradhi ya ugonjwa wa Covid 19 unaosababishwa na
virusi vya corona baada ya kuendelea kuua maelfu ya watu duniani, Mchungaji
Ambilikile Mwasapile maarufu kama Babu wa Loliondo ameibuka na kuiomba Serikali
kupeleka wagonjwa wa Corona kupata kikombe cha dawa.
Akizungumza jana Aprili 22, 2020 katika
mahojiano kwa njia ya simu na kituo cha redio cha Clouds Fm kupitia kipindi chake
cha Jahazi, Babu wa Loliondo amesema anashangazwa na ukimya ambao Serikali
imekuwa ikiufanya wakati yeye amekuwa akitoa dawa inayotibia magonjwa yote.
“Ndugu mtangazaji hii dawa
ninaitoa kwa masharti ya Mungu, na imekuwa ikitibia watu wengi sana na magonjwa
yote wanayoumwa, lakini tangu ugonjwa huu kuibuka nashangaa Serikali haileti
watu, mimi nawaomba walete watu wachache kwa majaribio wataona maajabu ya dawa
hii,” alisema.
Hata hivyo amesema hali ya ukimya
ambayo imekuwa ikiendelea kwa watu kutofika kunywa dawa kujitibia maradhi ya
corona umekuwa ukisababishwa na chuki ya baadhi ya watu dhidi yake ambao
wamekuwa wakimuonea wivu kwa kumtangazia mambo mabaya.
Alipotakiwa kuwataja watu hao
wabaya alisema muda ukifika atawaweka hadharani lakini kwa hivi sasa ataendelea
kukaa kimya na kwamba bado watumiaji wa dawa yake wataendelea kutoa Tsh500 kwa
kuwa bei hiyo ndio aliyooteshwa na kuagizwa kuitoza na sio vinginevyo. 
Aidha alipoelezwa kuwa ugonjwa wa
Corona hauruhusu watu kusafiri kwa kuwa utasababisha maambukizi mengi na hivyo
kwanini yeye asisafiri kuwapelekea dawa wagonjwa huko walipo, alisema kuwa
tangu alipooteshwa na Mungu na kupewa dawa hiyo aliagizwa iwe inatolewa
Loliondo katika eneo lake pekee na hivyo hatoweza kusafiri.
“kwanini  waendelee kufungia watu huko na wasiwalete
hapa kupata dawa? Kama mtu anaumwa sasa ni bora afungiwe au afike kunywa dawa?,”alihoji
Mchungaji Ambilikile Mwasapile.
Mchungaji Mstaafu wa KKKT, Ambilikile
Mwasapile maarufu kama ‘Babu wa Loliondo’ anayeishi katika mji wa Samunge
Loliondo, Wilayani Ngorongoro katika miaka ya karibuni amejipatia umaarufu
mkubwa baada ya kutangaza kuoteshwa kupata dawa ya kutibia maradhi yote sugu
ikiwemo Ukimwi, saratani na  sukari na
hivyo maelfu wa watu kutoka ndani na nje ya nchi kufika kwake kupata tiba hiyo.