Na Seif Mangwangi
APC Media
Balozi wa kampeni ya “MTU NI AFYA”, msanii Mrisho Mpoto,maarufu kama Mjomba amefika ofisi za Jiji la Arusha na kupokelewa na John L. Kayombo Mkurugenzi wa Jiji hilo.
Mrisho Mpoto amefika Jijini Arusha kwa lengo la kusaini hati ya makubaliano ya utendaji na utekelezaji wa kampeni ya “Mtu ni Afya” inayoratibiwa na Wizara ya Afya na Ofisi ya Rais-Tamisemi.

Kampeni hii ya Mtu ni Afya, ambayo ipo katika awamu ya pili,ilizinduliwa rasmi na Makamu wa Rais, Dkt.Philip Mpango Mei09, 024 imekuwa ikijikita katika maeneo tisa ikiwemo ujenzi wa vyoo bora na kuvitumia,unawaji mikono katika nyakati maalum.
Maeneo mengine ni usafi maeneo ya kazi na makazi,udhibiti wa utupaji taka hovyo,mazoezi ya mwili angalau dakika 30 kila siku,hedhi salama,Lishe bora,uandaji wa maji safi na salama ya kunywa na matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Aidha, Mrisho Mpoto ameeleza kuwa lengo kuu la kampeni ya Mtu ni Afya ni kujikita zaidi katika huduma za kinga badala ya kwenye tiba.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, John L. Kayombo amemhakikishia kumpa ushirikiano wa hali na mali na kumwambia kuwa kampeni hiyo imekuja wakati muafaka Jijini Arusha.
Kampeni hii imefanyika katika mikoa nane hapa nchini na sasa mkoa wa tisa ukiwa ni Arusha na utaratibiwa kwa kufanyika mikutano mitatu ya hadhara yenye lengo la kukumbusha jamii wajibu wa kubadili fikra za kujilinda kiafya.

