Baadhi ya wafanyakazi wa Kampuni ya Benson Security Systems na AfriTrack wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kuzindua mfumo wa kimtandao wa kudhibiti vyombo vya usafiri jijini Arusha |
Na Claud Gwandu, Arusha
TATIZO sugu la wizi wa pikipiki na vyombo vya moto huenda likawa historia mkoani Arusha na Tanzania kwa ujumla baada ya teknolojia mpya ya kudhibiti wizi huo kuzinduliwa.
Teknolojia hiyo itakayotumia mtandao wa mawasiliano wa internet imezinduliwa na Kampuni ya Benson ya jijini hapa ikishirikiana AfriTrack ya jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa Uendeshaji wa Kampuni ya Benson, Miqdaad Kassam alisema wakati wa uzinduzi huo kuwa,kwa kutumia teknolojia hiyo,pikipiki ikiibiwa, itapatikana kwa kuwa itaonekana iko wapi.
“Ni teknolojia rahisi itakayodhibiti wizi wa pikipiki ambao sasa ni moja ya matatizo sugu yanayolalamikiwa na wateja wengi.Ukifunga kifaa cha kudhibiti wizi katika pikipiki yako,hata kama ikiibiwa usiwe na wasiwasi,itapatikana tu,”alisisitiza Kassam katika uzinduzi huo.
Akifafanua, Mkuu wa Huduma kwa Wateja katika Kampuni hiyo, Salma Rothbletz alisema kifaa hicho maalum hfungwa katika pikipiki na kuunganishwa na simu yako ya mkononi ambako mteja hupata taarifa zote za uendeshaji wa pikipiki katika siku yake.
Aliongeza kuwa mfumo huo pia hudhibiti udanganyifu wa madereva katika matumizi ya mafuta na umbali aliotumia kwa siku katika uendeshaji wa pikipiki,jambo litakalowawezesha wamiliki wa pikipiki kuwa na uhakika wa mapato, kwa zile zinazofanya usafiri wa abiria.
“Mfumo huu utawasaidia wamiliki wa pikipiki za kusafirisha abiria kufuatilia biashara yao kwa ukaribu na uhakika kwa kuwa wanaweza kujua kiasi cha mafuta kilichotumika kwa siku na hata umbali ambao pikipiki imetembea,” alifafanua.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya AfriTrack, Suhail Sheriff alisema katika uzinduzi huo kuwa mtandao huo wa udhibiti wa vyombo vya usafiri unatumika pia katika malori na magari ya abiria na utasaidia kupunguza ama kuondoa kabisa ajali za barabarani.
Alisema mfumo huo hudhibiti hali ya dereva kama yuko timamu kuendesha chombo husika na iwapo kuna dosari hutoa ishara ya tahadhari kwa dereva mwenyewe na mwenye gari kabla ya madhara yoyote, ikiwa ni pamoja na ajali, kutokea.
“Kama gari lina hitilafu za kiufundi au dereva ana tatizo lolote, mathalan la kiafya, mfumo hugundua na baada ya muda hutoa ishara ya tahadhari unaosaidia hatua za kuzuia madhara yatokanayo na hitilafu hiyo kuchukuliwa haraka,”alisema Mkurugenzi Mtendaji huyo.
Kuhusu vyombo vya usafiri vinapokuwa katika maeneo yasito na mtandao wa mawasiliano,Sheriff alisema katika maeneo hayo, ikiwa ni pamoja na porini na bahari kuu ambako mawasiliano ni magumu,wanatumia mfumo wa mawasiliano wa setelaiti kufuatilia mwenendo wa vyombo hivyo katika maeneo hayo yasiyo na mtandao.
Sheriff alisema kuwa mfumo huo tayari unatumika kwa mafanikio makubwa katika nchi za Ivory Coast, Malawi,Zambia na sasa umeingia nchini katika miji ya Dar es Salaam, Arusha, Mwanza na Mbeya
Kwa upande wake Mwakilishi wa Kampuni ya Uhandisi ya Kiure, Omar Kiure alisema katika uzinduzi huo kuwa mfumo huo wa udhibiri magari na madereva katika sekta ya usafirishaji ni ukombozi kutokana na kukithiri kwa wizi hasa wa mafuta unaosababisha hasara kubwa.
“Wizi wa mafuta katika katika sekta ya usafirishaji na ujenzi ni sehemu ya tatizo sugu na linalokera mno katika sekta ya ujenzi na kwa kweli mfumo huu utatusaidia kudhibiti wizi huu unaotutia hasara mno na kusababisha gharama kuwa juu,” alisema Kiure.
Mwakilishi wa Jeshi la Polisi Mkoani Arusha, Atilio Choga alisema katika uzunduzi huo kuwa mfumo huo wa udhibiti utasaidia jeshi hilo kudhibiti na kupunguza au kumaliza kabisa tatizo la ajali za barabarani.