Bibi wa miaka 82 amtembezea kichapo kijana wa miaka 28

Bibi Willie Murphy wa miaka 82 ambaye alikuwa mtunisha misuli.

Bibi Willie Murphy mwenye umri wa miaka 82, kutokea jijini New York
nchini Marekani, amempiga mwanaume wa miaka 28, ambaye jina lake
halikuwekwa wazi kwa kosa la kuvamia nyumbani kwake bila ruhusa majira
ya saa 5:00 usiku.
Bibi huyo ambaye inadaiwa alikuwa anafanya michezo ya kutunisha misuli
‘Bodybuilder’ enzi za ujana wake, amesema alikuwa anaenda kulala
chumbani kwake, ghafla akasikia mtu anagonga hodi mlangoni huku akidai
kutaka kupigia gari la msaada wa wagonjwa lije nyumbani kwake.
Bibi huyo ameendelea kusema jamaa huyo aliamua kuvunja mlango wake na
kuingia ndani kwa nguvu na ndipo yeye alipojihami kwa kuwapigia simu
polisi, huku ameshika gongo na meza kisha kuanza kumpiga nazo jamaa
huyo.
Baada ya polisi kufika Bibi huyo alinukuliwa akisema “Ilikuwa ni usiku
na niko pekee yangu, mimi ni mzee, lakini wajua nini, nilichukua meza na
gongo nikampiga navyo, Polisi walivyoingia, tayari alikuwa amelala
chini kwa sababu nilikuwa nishamaliza kazi” amesema Bibi Willie Murphy.
Willie Murphy aliwahi kuwa mshindi wa mataji kadhaa ya michezo ya
kutunisha misuli na anaamini ujasiri alioufanya utawatia moyo watu wenye
umri kama wake.