- Apanga kugawa Taulo za kike kwa wanafunzi 10,000
Na Mwandishi Wetu
Arusha
Binti wa miaka 16 Arjun Kaur Mittal Mtanzania anayesoma Dubai katika nchi za Jumuiya ya Kiarabu (UAE), anatarajia kugawa taulo za kike kwa wanafunzi wa Sekondari za Serikali Jijini Arusha.
Arjun ambaye ameonyesha ujasiri na uwezo wa hali ya juu katika kusaidia Jamii isiyojiweza nchini anatarajia kuzindua zoezi la ugawaji wa Taulo hizo Agosti 11, 2024 katika viwanja vya hoteli ya TGT Jijini Arusha ambapo wageni mbalimbali wa ndani na nje ya nchi wanatarajiwa kuhudhuria.
Katika hafla hiyo ambapo wageni hao wamealikwa ambapo pia kutafanyika zoezi la kuchangia kampeni huyo, zaidi ya wasichana 10,000 wanatarajia kufikiwa lengo likiwa ni kuwaondolea usumbufu wa kukosa masomo kufuatia kukosa Taulo za kike pindi wanapongia kwenye siku zao.
Akizungumzia Binti Arjun Kaur Afisa programu kutoka wizara ya Afya, James Mhilu amesema, Binti huyo ni mfano wa kuigwa dhidi ya wasichana wengine nchini ambaye ameweza kuonyesha uwezo mkubwa wa kuwa kiongozi anayeweza kuibadilisha Jamii katika umri mdogo.
” Angalia katika umri mdogo tu wa miaka 16 Arjun ameweza kufanya mambo makubwa katika jamii, hili suala la kusaidia wasichana na kuwafanya kutimiza ndoto na malengo yao ni jambo kubwa sana katika maisha ya mwanadamu hasa Watoto wetu wa kike,” amesema na kuongeza:
” Wasichana wengi hasa wanaotoka familia duni wamekuwa wakikosa vipindi vya masomo kwa siku kadhaa kwa kila mwezi wawapo darasani pindi wanapoingia kwenye siku zao, lakini kwa msaada huu Sasa hivi wataondokana na kadhia hii,” amesema.
Amesema kuweza kuchangisha kiasi kikubwa Cha fedha Cha Dola zaidi ya elfu60 kununulia Taulo hizo ni jambo kubwa sana ambalo watu wengi wameshindwa kulifanya na zaidi ameweza kuonyesha moyo wake wa Upendo kwa wanafunzi wa kike.
” Arjun kwa umri mdogo wa miaka16 tu ameonyesha anaweza kufanya jambo kubwa kama hili, hii inaonyesha umri sio kitu endapo mtu atakuwa akitaka kufanya jambo fulani kwa jamii, hili ni somo kwa watoto wengine kujifunza na kuiga kutoka kwa binti huyu,” amesema Mhilu.
kwa upande wake Mkurugenzi wa kampuni ya kuunganisha magari ya HansPaul ya Jijini Arusha, Satbir amesema ameshangazwa na ujasiri aliokuwa nao Binti Arjun wa kuweza kufanya jambo kubwa kama hilo kwa jamii.
Amesema mradi huo ni muhimu sana kwa jamii kwa kuwa unaenda kuwaondolea wanafunzi wa kike adha ya kukosa masomo lakini pia kuwafanya kuwa na ujasiri na kujiona wao ni wathamani zaidi.
Katibu wa Chama Cha waendesha utalii nchini (TATO), Sirili Ako amesema maisha ya Watoto wa kike nchini hususani wanafunzi yamekuwa na vikwazo vingi ikiwemo kupata maradhi ya Afya ya uzazi kutokana na kukosa vifaa muhimu ikiwemo Taulo za kike jambo ambalo limekuwa likisababisha kukatisha masomo yao.
Amesema Arjun kwa umri mdogo aliokuwa nao ameweza kuwa na maoni makubwa sana nchini ambayo sio kila mtu anaweza kuyafanya na anaamini anaweza kuja kufanya mambo makubwa zaidi hapo baadae.
Sirili anasema anaamini Jamii yake ya watu wa Hanang Mkoani Manyara watakuwa ni miongoni mwa wafaidikaji wa msaada huo kufuatia wasichana wengi katika jamii hiyo kukatisha masomo yao na wengine kupata maradhi kwa kukosa elimu ya Afya ya uzazi.
Kwa mujibu wa Arjun kupitia taasisi yake ya Herneeds akishirikiana na taasisi za Lions Club, Alma Tanzania, SRLC na Software Pad watashirikiana kusambaza na kugawa taulo hizo za kike sambamba na kutoa elimu ya Afya ya uzazi na kuhusu matumizi sahihi ya Taulo hizo na umuhimu wa matumizi yake kiafya.
Tukio hili litakuwa sio la kwanza kwa binti Arjun ambapo akiwa na umri wa miaka 8 aliweza kukusanya fedha kwaajili ya kusaidia vituo vya Watoto yatima Jijini Arusha, pia amekuwa akitoa elimu ya michezo kwa watoto wadogo na ameweza kusaidia Vikundi vya wajasiriamali wanaotengeneza shanga kutengeneza Mtandao.
” Mwaka 2023 niliweza kutembelea soko la vinyago Arusha maarufu kama Masai Market ambapo niliweza kukutana na kina Mama na kuzungumza nao, niliwagawia Taulo za kike na kuwapatia elimu kidogo ya namna ambavyo wanaweza kufanya biashara na mwisho niliwasaidia kutengeneza tovuti inayokulikana kwa jina la www.masaimarkets.info, ili kujitangaza, “amesema.
Anasema Taulo hizo zitagaiwa kikanda ikiwemo kanda za Sombetini, Sinon, Kisongo, Njiro n.k na kwamba zoezi hilo litakuwa likifanyika kwa kila mwezi mara Moja ambapo timu itakayokuwa ikigawa itasambaza Taulo hizo kwa shule 3 hadi 5
” Kila mwezi baada ya mzigo wa Taulo kufika tutawapatia watu wetu wa kusambaza ambao watapeleka kwa kati ya shule 3 hadi 5 katika kila kanda, na kila aliyechangia atapata taarifa hii ili kuweka wazi zoezi zima,”amesema Arjun.