Ccm wampa onyo benard membe

Chama cha Mapinduzi (CCM) kimemuonya Benard Membe, kutokuwa juu ya katiba ya chama hicho.


Onyo
hilo limetolewa leo  na Dk. Bashiru Ally, Katibu Mkuu wa CCM, wakati
akizungumza katika mahojiano na kipindi cha Konani kinachorushwa na
Kituo cha ITV  kupitia mitandao yao ya kijamii.

Dk. Bashiru ameeleza kuwa, kama Membe ataendelea kutofuata utaratibu, uongozi wa chama hicho utamlazimisha kufuata utaratibu.

“Membe
ni mwanachama mwenye haki ya kikatiba lakini ana wajibu. Kwa hiyo kama
anataka kuwa mwanachama wa CCM kama walivyo wengine…  Asipofuata
utaratibu, atalazimishwa kufuata utaratibu,” ameeleza Dk. Bashiru.


“Membe hayuko juu ya katiba, Mwalimu Nyerere aliasisi CCM na hakuwa juu
ya katiba.  Membe akitaka kuwa mwanachama kama wengine wa CCM, afuate
utaratibu, asipofuata mimi ndiye msimamizi wa utaratibu huo
atalazimishwa kufuata utaratibu,” alisema.
Hata hivyo, amesema Membe hakuwahi kujadiliwa katika vikao vya chama,
licha ya kwamba hakuitikia wito wake, alipomtaka kuonana naye akiwa
mkoani Geita.
“Hatukuwahi kumjadili na kwenye vikao hakuwahi kufika. Kosa halifi kama
jinai, kosa halifi unaweza ukadhani limekufa kumbe ni utaratibu wa
wakati. Kupitia kwako, naomba kueleza wana CCM tuko makini kulinda
utamaduni wa chama, na wanachama kutii viapo vyao,” amesema Dk. Bashiru.
“Nimekuja kuimarisha chama na hasa kufunga mitambo ya ushindi mwaka
kesho, baada ya majaribio ya mitambo hiyo kufanya kazi kwenye uchaguzi
wa serikali za mitaa, natembea wilaya zote za Unguja na Pemba nikifunga
mitambo,” amesema Bashiru.