Ccm yakaribisha maoni ya mwelekeo wake wa sera na ilani ya uchaguzi

Chama
Cha Mapinduzi (CCM) kinapenda kuujulisha umma wa watanzania na
wanachama wa CCM kwamba kiko katika mchakato wa kuandika Mwelekeo wa
Sera za CCM kwa Mwaka 2020 hadi 2030 pamoja na uaandaji wa Ilani ya
Uchaguzi kwa Mwaka 2020 hadi 2025.Kama
ilivyo desturi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika michakato yake yote
ya uaandaji Nyaraka muhimu za Chama ikiwamo Mwelekeo wa Sera na Ilani ya
Uchaguzi Msingi Mkuu huwa ni ushiriki na ushikishaji wa umma wa
watanzania na wanachama wa CCM kote nchini. Msingi huu wa kushirikisha
umma unatokana na asili ya Chama ya Chama Cha Mapinduzi ambayo ni vitu
viwili, kutenda haki na kuheshimu watu.

Chama
kinawakaribisha mtu mmoja mmoja au vikundi vya watu na taasisi
mbalimbali ikiwemo lakini si kwa uchache, Vyama vya Wafanyakazi,
Wawakilishi na vyama vya Wakulima, Vyama vya Siasa vyenye Usajili wa
Kudumu, Vyama vya Waalimu, Wachimbaji wadogo wadogo wa madini,
wafanyabiashara wa madini, wawakilishi na vyama vya wakulima, wavuvi na
wafugaji, jumuia za wamachinga na wasafirishaji wadogo wadogo k.v.
bodaboda, bajaj n.k., Jumuia za wanawake, watu wenye ulemavu, vijana,
wazee, watoto, Asasi Zisizokuwa za Kiserikali (AZISE), wasomi, wanafunzi
wa vyuo na vyuo vikuu, wadau na wana tasnia ya Sanaa, burudani na
michezo, wasafirishaji wa mizigo na abiria, wenye viwanda, wadau wa
sekta ya utalii na vyama vya ushirika kwa maeneo yao.

Kwa
wanachama wa CCM Kamati za Siasa za Mikoa na Wilaya ziweke utaratibu wa
kukusanya maoni na kuwasilisha Makao Makuu kama ambavyo imekwisha
kuelekezwa.

Kamati
ya Uandishi wa Mwelekeo wa Sera na Ilani ya CCM chini ya Mwenyekiti
wake Mzee Phillip Japhet Mangula Makamu wa Mwenyekiti wa CCM Tanzania
Bara inaomba maoni haya yawe yamefika kwa Kamati kabla ya Tarehe 25
Januari 2020.

§ 
Maoni yanaweza kuwasilishwa kwa Ndg. Bashiru Ally, Katibu Mkuu wa CCM,
Makao Makuu ya CCM, S.L.P 50, Dodoma, Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM,
S.L.P 9151, Dar Es Salaam na Afisi Kuu ya CCM, Kisiwandui, Zanzibar, Na
kwa baruapepe: katibumkuu@ccm.or.tz

§  Maoni yanaweza pia kuwasilishwa kwa Ndg. Humphrey Polepole, Katibu wa Kamati ya Wataalam kupitia baruapepe: hpolepole@hpolepole.com

Uongozi
wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) chini ya Ndg. John Pombe Joseph Magufuli,
Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania unapenda
kuwatakia wana CCM na Watanzania wote Heri ya Mwaka Mpya, Mwaka 2020
ukawe wenye Baraka, Amani, umoja, neema, mafanikio na kuinuliwa kwa mtu
mmoja mmoja na Taifa la Tanzania, sote tukafanye kazi kwa bidii na huu
ukiwa ni msingi wa kulinda utu na uhuru wa Taifa letu.

Mungu Ibariki Tanzania na Watu wake,
Mungu Bariki Chama Cha Mapinduzi (CCM) na,
Mungu ubariki Mwaka 2020

KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI

Imetolewa na,


HUMPHREY POLEPOLE
KATIBU WA NEC – ITIKADI NA UENEZI
CHAMA CHA MAPINDUZI