Chama cha act-wazalendo chalalamika wagombea wake kuenguliwa bila sababu…kamati kuu ya chama hicho kukutana leo

Chama 
cha ACT-Wazalendo kimeeleza kufadhaishwa na kile kilichokiita hujuma
dhidi ya vyama vya upinzani katika uteuzi wa wagombea wa Uchaguzi wa
Serikali za Mitaa.


Akizungumza
na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kaimu Katibu Mkuu wa
chama hicho, Dorothy Semu, alidai kuenguliwa kwa wagombea wao,
kulipangwa mapema ili wagombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wapite bila
kupingwa.

“Wagombea wetu 110,040 nchi nzima wameenguliwa, wakiwamo 2,000 ambao hata sababu za kuenguliwa kwao hazijaelezwa.

“Kuenguliwa
kwa wagombea hawa na wengine kutoka vyama vya upinzani kumelenga
kuhakikisha wagombea wa CCM wanapita bila kupingwa,” alisema Semu.

Akifafanua
zaidi kuhusu kuenguliwa kwa wagombea wa chama chake, kiongozi huyo wa
ACT alidai baadhi ya wagombea wao wameambiwa hawana shughuli halali
licha ya kuwa miongoni mwa walipakodi wakubwa nchini.

Alidai
miongoni mwa walioenguliwa kwa kigezo hicho ni mgombea wao katika Mtaa
wa Masaki jijini, ambaye jina lake limekatwa licha ya kuwa ni
mfanyabiashara anayetambuliwa na Mamlaka ya Mapato (TRA) na hulipa kodi
ya zaidi ya Sh. milioni 30 kwa mwaka.

Alidai
kuna wagombea wao wameenguliwa kwa kuelezwa kuwa chama hicho hakipo
katika orodha ya vyama vilivyosajiliwa kwa msajili wa vyama nchini.

Semu
pia alisema kuna walioenguliwa kwa madai kuwa si wakazi wa maeneo
wanayogombea licha ya kuzaliwa katika maeneo hayo na kuwa na makazi ya
kudumu na familia zao kuishi katika maeneo husika.

“Kuna
hujuma pia ilifanyika kwa fomu za wagombea wetu kughushiwa na kuongezwa
herufi za majina ya mgombea na hivyo mgombea kuenguliwa kwa maelezo
kuwa majina yaliyotumika siyo sahihi licha ya kuwa fomu hizo zilijazwa
majina sahihi,” alidai.

Alisema
tayari chama hicho kimeanza kuchukua hatua dhidi ya suala hilo kwa
kufanya mawasiliano na vyama vingine, vikiwamo Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema), National League for Democracy (NLD) na Chama cha
NCCR-Mageuzi ili kuunganisha nguvu na kuchukua hatua za pamoja.

Aliongeza
kuwa kamati ya chama imeitishwa kwa dharura na itakuwa na kikao leo ili
kutafakari hatua za kuchukua kukabiliana na kile alichoita hujuma dhidi
ya vyama vya siasa nchini.