Corona yaibua mapya, wanafunzi waolewa, wapewa mimba ngorongoro

NA MWANDISHI WETU, APC BLOG, NGORONGORO

Loliondo

ZAIDI ya Wanafunzi 12  wa shule za Msingi na Sekondari Wilaya ya Ngorongoro Mkoa wa Arusha, wamepewa ujauzito  na wengine kuolewa kati ya Januari hadi April mwaka huu 2020.

Wanafunzi katika moja ya shule ya msingi Ngorongoro


Uchunguzi uliofanywa na waandishi wa APC Blog kwa kishirikiana na taasisi ya Msichana Initiative na Mimutie Woman Organization  na kuthibitishwa na  viongozi wa Halmashauri ya Ngorongoro,  umebaini kuwa wimbi la watoto kupata ujauzito limechangiwa na watoto wa kike kuwa nyumbani kutokana na ugonjwa wa Corona.

Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Ngorongoro, Emmanuel Sukums,alisema kuna tatizo kubwa katika jamii ya wakazi wa Ngorongoro, kutothamini elimu na hivyo kuwaondoa shule watoto.

Amesema baadhi ya wazazi wanashirikiana na watuhumiwa kujikinga na vyombo Vya dola.

Mkurugenzi wa shirika la MIMUTIE, Rose Njilo alisema wanaomba serikali kuongeza ufatiliaji wa wanafunzi wa kike kwani, kama hatua zisipochukuliwa zaidi ya nusu ya wanafunzi wa kike wa sekondari na msingi wanaweza kutorejea shuleni kutokana na ujauzito na kuolewa.

“sisi kama Mimutie na Msichana Initiative tumeona kuna tatizo kubwa, sasa baadhi ya vijana wameona ugonjwa wa Corona uliosababisha watoto kurudi majumbani ni fursa ya kuwapa mimba na kuwaowa watoto tunataka hatua za kisheria kuchukuliwa”alisema

Amesema wasichana initiative na Mimutie zitaendelea kupinga matukio ya kupewa mimba watoto na inataka polisi na mahakama kusaidia kutokomeza matukio hayo.

Afisa Maendeleo ya jamii wilaya ya Ngorongoro,Benezeth Bwilizo alisema tayari wamepokea taarifa za wanafunzi wanne wa shule ya msingi kupewa ujauzito na wanafunzi sita wa sekondari.

“hili tatizo bado ni kubwa, kwani mwaka jana tulipata kesi za wanafunzi kupewa mimba zaidi ya 20, tunaendelea kupambana na mila potofu za kutosomesha watoto wa kike na kuolewa wakiwa bado wadogo”alisema

Mmoja wa wanafunzi mkazi wa Kata ya Olorieni Magaiduru, ambaye alikuwa anasoma kidato cha kwanza shule ya sekondari Wasso(jina linahifadhiwa) alikiri kupewa ujauzito .

Mwanafunzi huyo,aliomba serikali kumsaidia ili aweze kuendelea na masomo ya sekondari kwani, hana lengo la kuolewa sasa kwani anataka kuja kuwa mwalimu kama akiendelea na masomo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *