Corona yaifundisha jamii nidhamu ya usafi

 

Na Mwandishi Wetu, Arusha.

Licha ya ugonjwa wa
homa kali ya mapafu (Covid-19) kuleta taharuki katika jamii lakini kwa upande
mwingine imesaidia kuielimisha jamii umuhimu wa usafi kama vile kunawa mikono
kila mara ikiwa ni pamoja na kutogusana kiholela.

Kauli hiyo imetolewa na
baadhi ya wakazi wa mji wa Arusha walipozungumza na APC Blog juu ya athari ya
ugonjwa huo ambapo walisema licha ya kuwa ulileta taharuki katika jamii lakini
umesaidia kutoa elimu ya afya ambayo wataendelea kuizingatia siku zote.

“Kwa kweli tulizoea
kuishi maisha ambayo kiafya hayakuwa salama, kumbe hatupaswi kushikana mikono,
kupiga chafya au kukohoa bila kuziba mdomo kwa mitambaa au mikono, lakini pia
tulikuwa hatufahamu kama misongamano siyo salama kiafya” Alisema mama Vivian
mfanyabiashara wa chakula maarufu kama ntilie katika soko la Mbauda.

“Mfano kama mteja
anakula chakula ambacho haitaji kutumia mikono tulikuwa tunampatia kijiko
anaendelea kula, lakini kwa sasa uwe unakula kwa kijiko, mkono au unataka tu
kuingia ndani kuulizia bei ya chakula, ni lazima unawe kwenye ndoo hiyo hapo
nje ndo uingine ndani uhudumiwe” Aliongeza

Kwa upande wa wauza
nguo za mitumba katika eneo la Manzese nao wamesema wanahakikisha kila mteja anayefika
eneo la baishara zao wanampa dawa ya kutakasa mikono (sanitizer) ndiyo aendelee
kuchagua nguo.

Mmoja wa wafanya
biashara wa nguo hizo za mitumba Abdul Komu amesema hali hiyo itakuwa endelevu
kwani wameshajua umuhimu wa afya kwa kuwa inawasaidia kuwakinga na magonjwa
mengi tofauti na CORONA.

APC Blog imeshuhudia
maafisa afya kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Jiji wakipita katika kituo cha
daladala Kilombero na kutoa elimu ya unawaji wa mikono hasa kwa abiria
wanaotumia usafiri huo kuhakikisha hawapandi bila kuna mikono.

“Hakikisheni kila
daladala mnayopanda mnapewa maji ya kunawa au kitakasa mikono, sisi maafisa
afya tumetoa dawa ya kuweka kwenye maji kwa kila gari, kwa hiyo msiogope
mkasema mbona haya maji hayana sabuni. Hivyo hakikisheni mnatunza afya zenu kwa
hiari msisubiri kulazimishwa” Alisema mmoja wa maafisa afya ambaye alisema
hawezi kutaja jina lake kwa kuwa yeye siyo msemaji wa suala hilo.