Corona yakwamisha mapambano dhidi ya malaria: who

 Na Mwandishi Wetu, Arusha

Wakati mlipuko wa ugonjwa wa homa ya Mapafu ( Covid – 19), ukielezwa kumalizwa nchini kutokana na jitihada mbalimbali zilizofanywa na Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt John Pombe Magufuli, shirika la Afya Duniani, limesema ugonjwa huo ambao umeendelea kuua maelfu wa watu duniani unakwamisha mapambano dhidi ya ugonjwa wa Malaria.

Shirika la WHO limeonya kuwa kutokana na
kulishughulikia zaidi janga la virusi vya corona huenda kukawa na hadi vifo
100,000 zaidi vitokanavyo na ugonjwa wa malaria kwa mwaka huu.

 

Katika ripoti yake ya mwaka
kuhusu ugonjwa wa malaria duniani iliyotolewa Novemba 30, 2020, WHO imesema
maendeleo ya kupambana na ugonjwa huo yamekwama katika miaka ya hivi karibuni
hasa katika eneo la Kusini mwa Jangwa la Sahara, ambako kuna visa vingi pamoja
na vifo.

Mbu aina ya anopheles wa kike. mbu huyu ndio anayeambukiza ugonjwa wa Malaria

 

WHO imesema mwaka 2019 kulikuwa
na takriban maambukizi milioni 229 ya malaria duniani, takwimu ambazo zilikuwa
sawa na za miaka minne iliyopita na kwamba vifo vya malaria vinaweza kuzidi
vile vitokanavyo na janga la COVID-19, huku wengi wao wakiwa watoto.

 

Kwa mujibu wa shirika hilo, watu
409,000 duniani walikufa kwa ugonjwa wa malaria mwaka 2019, wengi wao wakiwa
kutoka maeneo masikini ya Afrika, ikilinganishwa na watu 411,000 kwa mwaka
2018.

 

Hata
hivyo, ripoti hiyo imesema kuwa kampeni nyingi za kupambana na malaria
ziliendelea wakati huu ambapo janga la virusi vya corona limeendelea kuua
maelfu wa watu duniani, lakini kuna wasiwasi kwamba juhudi za kukabiliana na
malaria zinaingiliana na mzozo wa COVID-19 ambao unakwamisha juhudi hizo na
kurudisha nyuma zaidi mapambano.

 

Mkurugenzi wa WHO anayehusika na
mpango wa malaria, Pedro Alsonso, amesema kutokana na mzozo wa corona, nchi
nyingi zimefunga mipaka yake na viwanda hatua ambayo pia inazuia au inakwamisha
kupelekwa kwa vyandarua vya kujikinga na mbu pamoja na dawa za malaria.

 

Aidha, serikali zimezielekeza
rasilimali zake katika kupambana na janga la COVID-19, ambazo pia zilikuwa ni
gharama za kupambana na malaria.

Mkurugenzi wa WHO barani Afrika,
Matshidiso Moeti amesema virusi vya corona vinatishia kukwamisha juhudi za
kupambana na malaria. Moeti amesema licha ya COVID-19 kuuathiri uchumi wa
Afrika, washirika wa kimataifa wanahitaji kuongeza juhudi kuhakikisha kwamba
rasilimali zinaongezwa katika miradi ya malaria ambayo inaleta mabadiliko.

 

Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Tedros
Adhanom Gebreyesus amesema ni muda kwa viongozi wa Afrika na dunia kwa ujumla
kuamka tena na kupambana na malaria. WHO imesema upungufu wa fedha za kupambana
na malaria unaleta kitisho kikubwa, huku ikiwa na dola bilioni 3 kati ya dola
bilioni 5.6 zilizochangishwa 2019.

 

Zaidi ya asilimia 90 ya ugonjwa
huo uko barani Afrika, ambapo takwimu zinaonyesha watu 384,000 walikufa mwaka
uliopita 2019 huku nchi kama Nigeria ikitajwa kuwa na asilimia 27 ya vifo
hivyo, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo asilimia 12, Uganda asilimia tano na
Msumbiji asilimia nne.

 

Kwa mujibu wa aliyekuwa waziri wa
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na watoto Ummy Mwalimu alipokuwa akiwasilisha
bajeti ya Wizara Juni mwaka huu, 2020,
Maambukizi ya Malaria yamepungua
kutoka asilimia 14.8 mwaka 2015/16 hadi kufikia asilimia 7.3 Machi 2020. Aidha,
vifo vitokanavyo na malaria vimepungua kutoka vifo 6,311 mwaka 2015 hadi
kufikia vifo 2,079 Machi 2020.

 

Aidha ripoti ya WHO imesema nchi
21 zimefanikiwa kuutokomeza ugonjwa wa malaria katika kipindi cha miongo miwili
iliyopita. Nje ya Afrika, India imeendelea kupata faida kubwa katika miaka
miwili iliyopita, huku ikipunguza asilimia 18 ya maambukizi na asilimia 20 ya
vifo.

 

Peter Sands, Mkurugenzi Mkuu wa
mfuko wa dunia wa kupambana na UKIMWI, kifua kikuu na malaria amesema ripoti ya
WHO imetolewa kwa wakati unaofaa.

 

Hata hivyo wakati WHO ikitoa
takwimu na taarifa yake, nchini ugonjwa wa Malaria umeendelea kuthibiwa kwa hatua
mbalimbali ikiwemo kunyunyiziwa kwa dawa kwenye mazalia ya mbu katika maeneo
ambayo yameonekana kuwa hatarishi.