Dc mwegelo : chagueni viongozi wa kuendana na kasi ya rais magufuli

Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Joketi Mwegelo
Na Shushu Joel
Mkuu wa wilaya ya Kisarawe ambaye
anakaimu Ukuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Mhe. Joketi Mwegelo amewataka
wananchi wa Halmashauri ya Chalinze kuwachagua viongozi wenye utayari na
uwezo wa kuendana na kasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Dkt. John Pombe Magufuli.


Rai hiyo ameitoa wakati akizungumza na wakazi wa kata ya Bwilingu kwenye viwanja vya kituo cha mabasi cha Barabara ya Morogoro.

Mkuu huyo wa wilaya aliwakumbusha na
kuwasisitiza wananchi hao kutambua dhamana kubwa waliyonayo na yupi ni
kiongozi atakayekuwa ni kiungo kikubwa kwa viongozi wa juu na anayeweza
kuendana na utendaji wa Rais Magufuli.

Pia Mkuu huyo wa wilaya aliwataka
wananchi kuendelea kujitokeza kwenye zoezi la kujiandikisha kwenye
daftari la kupiga kura huku akiwapa msisitizo kuwa ni wale watakaokuwa
kwenye orodha ndani ya daftari la wapiga kura tu ambao watapata fursa ya
kupiga kura.

 “Wananchi wenzangu wale ambao wanadhani
kuwa kile kitambulisho cha kupiga kura kitawawezesha kushiriki uchaguzi
huu, hapana. Uchaguzi huu tunatumia daftari hivyo ni muhimu kwenda
kujiandikisha”.

“Jambo la kuwa na vitambulisho kuwa kigezo si kweli bali ni wewe tu kuweza kufika kituoni na inakuchukua dakika 2 tu”,alisema.

Katika hatua nyingine,Mhe, Mwegelo
amempongeza Mbunge wa jimbo la  Chalinze Mhe. Ridhiwani Kikwete kwa
utekelezaji na ufanikishaji wa miradi mbalimbali katika jimbo lake na
jinsi alivyojitokeza yeye akishirikiana na wananchi kuhamasisha
uandikishaji.

Aidha amewataka wananchi hao kuwa na
viongozi watakaochaguliwa kwenye vitongoji na vijiji wawe wachapakazi
kwa ajili ya kufanya kazi nzuri ya kuleta maendeleo.

“Ninyi wenyewe mashuhuda na Mbunge
ameeleza jinsi Miradi mikubwa kama ya maji,afya,madarasa, miundombinu na
umeme ilivyotekelezwa kwa asilimia kubwa sana. Nakupongeza Mhe. Mbunge
kwa utekelezaji mzuri wa majukumu”,alisema.

Naye mzee Zaidi Lufunga (78) akizungumza
kwa niaba ya Wana Chalinze amempongeza mkuu huyo wa wilaya kwa kujionea
mafanikio makubwa yaliyofanywa na serikali ya awamu ya tano katika
jimbo la Chalinze.

“Miaka yetu changamoto zilikuwa nyingi
sana, lakini kipindi hiki cha Rais Magufuli kwa kushirikiana na mbunge
wetu Ridhiwani Kikwete mafanikio tunayapata na kazi nzuri inaonekana.
Kutokana na utekelezaji wa miradi mikubwa na iliyokuwa ndiyo ndoto zao
ni tu tutachagua viongozi wenye hofu ya Mungu”,alisema Mzee Lufunga.

Kwa upande wake mbunge wa jimbo la
Chalinze Mhe. Ridhiwani Kikwete amempongeza mkuu huyo wa wilaya kwa ujio
wake wa kujionea jinsi Wanachalinze wanavyojitokeza katika zoezi la
kujiandikisha.

Amewapongeza wakazi wa kata ya Bwilingu
kwa kujitokeza kwa wingi ili kumsikiliza mkuu wa wilaya akieleza kuwa
hilo ni jambo kubwa na kwa hakika linatoa dalili kuwa wananchi wako
tayari. 

Hadi kufikia jana Halmashauri ya
Chalinze ilikuwa imefikia Asilimia 74 ya Uandikishaji na baada ya
kukatika kwa mvua kumekuwa na wingi wa wananchi kujiandikisha. Zoezi
hili linatarajiwa kuisha tarehe 17 Oktoba ambapo matarajio ya
kuandikisha watu 136,000 utafikiwa huku hadi jana watu zaidi ya 90,000
wakiwa wamejitokeza kujiandikisha.


Mbunge wa jimbo la Chalinze Mhe,
Ridhiwani Kikwete akizungumza na wakazi Bwilingu juu ya kujiandikisha
kwenye daftari la kupiga kura.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *