Dc ole sabaya aagiza tanesco kukata umeme ofisi za halmashauri ya wilaya ya hai

Mkuu
wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya, ameagiza kukatwa umeme  ofisi za
Halmashauri ya Wilaya ya  Hai, mahali ambapo ofisi yake pia ipo hapo,
kwa kile alichokieleza Halmashauri hiyo haijalipa bili ya Soko Kuu la
Hai kwa muda wa miezi 2, na kuitaka TANESCO wakawashe umeme kwenye soko
hilo.

Alitoa
agizo hilo jana baada ya kutembelea soko hilo akimtaka Meneja wa
Shirika la Umeme (Tanesco) kurejesha huduma ya umeme sokoni hapo
iliyoondolewa na shirika hilo kutokana na halmashauri kutolipa bili.

“DED
(Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya) na watu wako mnakuja kukusanya
fedha kwa miezi mitatu mfululizo, mnasahauje kulipa bili kupitia fedha
hizo?

“Hili
nalo Rais asimamishwe aambiwe? Mimi na wewe tuwaombe radhi hawa
wananchi, ila wakati huo nakuagiza Meneja wa Tanesco ukate umeme Ofisi
ya Mkurugenzi na uwashe hapa sokoni na alipe deni hilo, na alipe bili za
miezi sita ijayo.

“Umeme
uwake hapa leo (jana) na ‘go ahead’ (maelekezo) ya kuwasha umeme kwa
DED nitakupa baada ya kuona risiti. Na kwa kuwa ofisi yangu iko kwenye
jengo hilo (la DED) tukapambane wote na hilo joto la kuwapuuza hawa
wananchi tunaoambiwa kila siku kuwasikiliza na kuwahudumia.”

Hata
hivyo, Ole Sabaya alimweleza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo,
Yohane Sintoo, kuwa hayuko tayari kufanya kazi kwenye ofisi ambayo haina
huduma ya umeme na hayuko tayari kuona wananchi wanatozwa kodi ambayo
hairudi kulipa deni la umeme.

Kutokana
na agizo hilo, Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo (Sintoo) alikiri kuwapo
kwa changamoto hiyo na kuwaomba radhi wananchi kutokana na kukatwa kwa
umeme kwenye soko hilo.