Elimu ya kodi yawafikia wafanyabiashara na wananchi wa malinyi

Afisa Kodi Mkuu wa Mamlaka ya
Mapato Tanzania (TRA), Bw. Julius Mjenga akiwaelimisha baadhi ya
Wafanyabiashara wa Wilaya ya Malinyi mkoani Morogoro wakati wa Wiki ya
Huduma na Elimu kwa Mlipakodi kwa Mikoa ya Morogoro na Pwani.




Baadhi ya Wafanyabiashara wa
Wilaya ya Malinyi mkoani Morogoro wakisikiliza elimu ya kodi kutoka kwa
Afisa Kodi Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Julius Mjenga
(hayupo pichani) wakati wa Wiki ya Huduma na Elimu kwa Mlipakodi kwa
Mikoa ya Morogoro na Pwani.


Baadhi ya Wafanyabiashara wa
Wilaya ya Malinyi mkoani Morogoro wakijisomea kitabu cha Kodi na Ushuru
Mbalimbali wakati wa Wiki ya Huduma na Elimu kwa Mlipakodi kwa Mikoa ya
Morogoro na Pwani.(PICHA ZOTE NA TRA)


Na Veronica Kazimoto-Malinyi

 Mamlaka
ya Mapato Tanzania (TRA) imekutana na wafanyabiashara pamoja na
wananchi wa Wilaya ya Malinyi mkoani Morogoro kwa ajili ya kutoa elimu
ya kodi ikiwa ni pamoja na kuwasajili wafanyabiashara wasiokuwa na Namba
ya Utambulisho wa Mlipakodi.

Akizungumza na
wafanyabiashara hao wakati wa utoaji wa elimu hiyo, Afisa Kodi Mkuu wa
TRA, Julius Mjenga, amewahimiza kutunza kumbukumbu za biashara zao ili
kukadiriwa kodi stahiki.

“Mara nyingi
wafanyabiashara wamekuwa wakilalamika kuwa TRA inawakadiria kodi kubwa
lakini mlio wengi hamtunzi kumbukumbu kwenye daftari linaloonyesha
manunuzi na mauzo ya kila siku ili mwisho wa mwaka Afisa wa Kodi atumie
daftari hilo kukukadiria kodi ambayo inaendana na uhalisia wa biashara
yako,” alisema Mjenga.

Mjenga
ameongeza kuwa, mfanyabiashara anaetunza kumbukumbu analipa kodi kidogo
ukilinganisha na mfanyabiashara ambaye hatunzi kabisa kumbukumbu za
biashara yake.

Naye
mfanyabiashara wa vifaa vya ujenzi, Samson Nyanda wa wilayani hapa,
ameiomba TRA kutoa elimu ya kodi mara kwa mara kwa kuwa wafanyabiashara
huongezeka kila wakati.

“Elimu hii
tuliyoipata ni nzuri mno ila tunaomba iwe endelevu na ifanyike hata kwa
mwaka mara tatu kwa sababu kila wakati wafanyabiashara wanaongezeka na
wengi wao hawana hii elimu ya utunzaji wa kumbukumbu”, alieleza Nyanda. 

Mamlaka ya
Mapato Tanzania inafanya Kampeni ya Elimu, Usajili na Huduma kwa
Mlipakodi katika Mikoa ya Morogoro na Pwani ambapo kwa Mkoa wa Morogoro,
timu ya maafisa wa TRA inatarajia kuwafikia wafanyabiashara na wananchi
wa Kilosa, Ulanga, Kilombero, Mvomero, Gairo na Morogoro vijijini.

Wakati katika
Mkoa wa Pwani, timu ya maafisa wa TRA imelenga kuwafikia wafanyabiashara
wote wa maeneo ya Kibaha, Kibiti, Kisarawe, Mkuranga, Chalinze na
Bagamoyo ambapo kampeni hiyo imeanza tarehe 11 na itamalizika tarehe 17
Novemba, 2019.