Elimu ya manufaa ya hatimiliki za kimila itolewe kwa walengwa wa mkurabita

Na. Aaron Mrikaria –
Rungwe

Watendaji wa
Halmashauri zinazonufaika na Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za
Wanyonge Tanzania (MKURABITA) watakiwa kubeba dhamana ya kutoa elimu kuhusu
manufaa ya hatimiliki za kimila ili walengwa wa mpango huo wanufaike kupitia
hati hizo.
Wito huo umetolewa jana
na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,
Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) kwa Watendaji wa Halmashauri akiwa katika ziara
ya kikazi Wilayani Rungwe yenye lengo la kukagua  utekelezaji wa miradi ya MKURABITA.
Mhe. Dkt. Mwanjelwa
amesema nimetembelea miradi ya MKURABITA iliyopo katika baadhi ya Halmashauri na
kugundua kuwa Watendaji wa Halmashauri ilipo miradi hiyo hawatekelezi wajibu wao
wa kuwaelimisha wananchi juu ya umuhimu wa kurasimisha raslimali na biashara zao.
“Mkurugenzi na Mwenyekiti
wa Halmashauri hakikisheni katika mpangokazi wenu mnaliwekea kipaumbele suala la
elimu kuhusu MKURABITA kwa sababu lina manufaa kwa wananchi ambao Mhe. Rais,
Dtk. John Pombe Magufuli amekuwa mstari wa mbele kuwawezesha”.  
Aidha, Dkt. Mwanjelwa amezishukuru
baadhi ya taasisi za kifedha kwa kutambua Hatimiliki za Kimila na kutoa mikopo ya
zaidi ya shilingi milioni mia tisa kwa wakulima wa chai wa Wilaya hiyo, ikiwemo
Benki ya CRDB, NMB na SACCOS ya kijiji cha Ntandabala. 
Mratibu wa MKURABITA, Dkt.
Serafia Mgembe amesema wananchi waliopata hatimiliki za kimila wanakabiliwa na changamoto
ya kutokujua namna ya kuzitumia hati hizo kupata mikopo ikiwemo ujuzi wa kubuni
miradi na namna ya kuandika mpangokazi wa 
kuombea mkopo.
Dkt. Mgembe amezishauri
taasisi za kifedha zifungue dirisha la kutoa elimu kwa wananchi ili iwe rahisi kwao
kutambua namna wanavyoweza kupata mitaji na kujiendeleza kiuchumi.
 

Naibu
Waziri  Ofisi ya Rais Menejimenti
ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mheshimiwa Dkt. Mary Mwanjelwa akizungumza
na  wanakijiji wa Ntandabala kata
ya Masoko Wilayani RUNGWE katika ziara ya kikazi ya kukagua mradi wa
kurasimisha raslimali za wanyonge ( MKURABITA).



Baadhi
ya Wazee na Vijana wa kijiji cha Ntandabala kilichopo Kata ya Masoko Wilayani
Rungwe Mkoani Mbeya wakimsikiliza, Naibu Waziri  Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala
Bora Mheshimiwa Dkt. Mary Mwanjelwa 
alipokuwa akitoa ufafanuzi juu ya uamuzi wa serikali kuanzisha mpango wa
kurasimisha raslimali za wanyonge (MKURABITA) na faida zake kwa wanufaika

Baadhi
ya akina Mama wa Kijiji cha Ntandabala kilichopo kata ya Masoko Wilayani Rungwe
wakimshukuru  Naibu Waziri  Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi
wa Umma na Utawala Bora Mheshimiwa Dkt. Mary Mwanjelwa kwa kufanya ziara
kijijini hapo na kutoa  maelekezo
yatakayowasaidia kutatuliwa kero zao za kurasimishiwa maeneo yao na kunufaika
na mikopo katika taasisi za fedha.

Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb)
yuko mkoani Mbeya katika ziara ya kikazi ya kukagua utekelezaji  wa Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na
Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA).