Hospitali ya Mount Meru yaleta Madaktari Bingwa 30, Kutibu wagonjwa 4000 bure

  • Ni kwa wagonjwa wa huduma za kibingwa na magonjwa sugu
  • Mamia wafurika, magonjwa yasiyoambukiza yashika kasi

Na Seif Mangwangi, APC MEDIA

Arusha

HOSPITALI ya rufaa ya Mkoa wa Arusha ,Mount Meru imezindua kampeni ya siku nne ya kutoa bure matibabu ya kibingwa kwa wakazi wa Mkoa wa Arusha ikiwa ni katika kuunga mkono juhudi za Rais Dkt Samia Suluhu Hassan katika kuboresha sekta ya Afya nchini  pamoja na maadhimisho ya miaka 63 ya Uhuru

Akizungumza katika viwanja vya hospitali hiyo leo Disemba 6, 2024 Daktari Mfawidhi wa Hospitali hiyo Dkt. Alex Ernest amewataka wakazi wa Arusha popote pale walipo wafike hospitalini hapo kwaajili ya kupata huduma za kitabibu bila kulipia chochote.

Amesema katika kampeni hiyo, zaidi ya madaktari bingwa 30 watakuwepo ambapo hadi kukamilika kwa zoezi hilo Disemba 9, 2024 wanatarajia jumla ya wakazi 4000 wa jiji la Arusha wataweza kupata tiba za kibingwa ikiwa ni wastani wa wagonjwa 1000 watakuwa wakitibiwa kwa siku.

“Tunawatangazia wakazi wote wa Arusha wanaosumbuliwa na maradhi mbalimbali wafike hospitalini hapa kwaajli ya kupata tiba ya bure, wataweza kuwaona madaktari bingwa na kuhudumiwa kwa uangalizi wa hali ya juu,”amesema.

Amesema wagonjwa watakaolazimika kufanyanyiwa upasuaji, watalazwa na kupewa huduma hiyo bure katika hospitali hiyo lakini watakaolazimika kupewa rufaa hao watajigharamia huko watakapohamishiwa kwa kuwa huduma za bure ni katika hospitali hiyo pekee.

wagonjwa katika hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Arusha Mount Meru wakisubiria kupata huduma za kibingwa katika kampeni maalum iliyoanza leo hospitalini hapo

Dkt Ernest amesema zaidi ya huduma 15 zitatolewa kupitia madaktari bingwa hao ikiwemo huduma za mama na mtoto, magonjwa ya mfumo wa mkojo, kinywa ikiwemo pua na masikio, meno, macho, ngozi, kisukari, huduma za mifupa, pathologia, magonjwa yasiyoambukiza kama saratani, shiniko la damu n.k.

Amesema magonjwa yasiyoambukiza yamekuwa ni changamoto kubwa nchini kwa kuwa waathirika wamekuwa wakigundua kuwa nayo wakati ugonjwa ukiwa umeshasambaa kwa kiasi kikubwa kutokana na kutokuwa na tabia ya kupima afya mara kwa mara.

“Kupitia kampeni hii pia tutakuwa tukitoa elimu kwa wagonjwa kuhusiana na mfumo wa maisha ili kuweza kubadili mfumo wao wa maisha wanaoishi ambao ndio umekuwa ukisababisha magonjwa mengi yasiyoambukiza,”amesema.

Dkt Ernest amesema pia kampeni hiyo imeletwa ili kutaka wananchi kujionea namna serikali ilivyowekeza kwenye sekta ya afya nchini kwa kufanya mapinduzi makubwa ikiwemo ununuzi wa vifaa vya kisasa vya maabara.

“Lakini lengo lingine ni kutaka kufikia wananchi wale wasiokuwa na uwezo wa kupata huduma za kibingwa kutokana na changamoto nyingi ikiwemo gharama zake kuwa kubwa kuweza kuzipata, pia kusogea karibu huduma kwa wananchi,”amesema.

Mganga mfawidhi wa hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Arusha Mount Meru Dkt Alex Ernest akizungumza na mmoja wa wagonjwa waliofika kupata huduma